Ligi Kuu

Fountain Gate, Pamba Jiji kukatana Arusha

ARUSHA: FOUNTAIN Gate na Pamba Jiji zinatarajiwa kuvaana leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, mkoani Arusha, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara unaozikutanisha timu hizo zikiwa na malengo ya kupata alama muhimu.

Fountain Gate inaingia katika mchezo huo ikitaka kutumia faida ya uwanja wa nyumbani kujipatia alama zitakazoisaidia kujiweka katika mazingira mazuri zaidi ya kuendelea na ushindani wa ligi hiyo.

Kocha wa timu hiyo, Fred Minziro, amesema anatambua ubora wa Pamba Jiji na aina ya kikosi watakachokabiliana nacho, lakini amesisitiza kuwa wanahitaji matokeo mazuri mbele ya mashabiki wao.

“Nafahamu ubora wa Pamba na ni timu nzuri, hivyo najua tunaenda kuikabili timu ya aina gani. Hata hivyo, sisi tupo nyumbani na tunahitaji alama ili kujenga mazingira mazuri zaidi,” amesema Minziro.

Amesema benchi lake la ufundi limefanya marekebisho katika safu za ulinzi na ushambuliaji, huku jukumu kubwa likibaki kwa wachezaji kutekeleza maelekezo waliyopata wakati wa mazoezi ili kupata matokeo wanayoyahitaji.

Kwa upande wa Pamba Jiji, kocha Francis Baraza anakabiliwa na changamoto ya muda mfupi wa maandalizi kutokana na safari ndefu pamoja na majeraha ya wachezaji yaliyopunguza idadi ya chaguo katika kikosi chake.

Baraza amesema baada ya mchezo uliopita, timu yake ilipata siku moja tu ya kufanya mazoezi mepesi, huku akieleza kuwa mapumziko ya mechi za kimataifa yalimpa nafasi ya kufanya maandalizi ambayo kwake yalikuwa sawa na maandalizi ya awali ya msimu.

Hata hivyo, kocha huyo anaamini Pamba Jiji inaweza kutoa ushindani dhidi ya Fountain Gate, akisisitiza kuwa wapinzani wao ni timu nzuri ambayo haipaswi kudharauliwa. Alikumbusha pia kuwa msimu uliopita Pamba Jiji iliifunga Fountain Gate bao 1-0 katika michezo yao ya nyumbani na ugenini.

Timu zote mbili zimechika mkia kila mmoja ana pointi nne, wote wanahitaji matokeo mazuri kusonga mbele.

Mchezo mwingine utakaochezwa leo ni Geita Gold dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Bukombe Geita.
Mwisho

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button