Africa

Singia, Tusker kufukuzia Kombe la Shirikisho Afrika

KENYA: TUSKER FC ya Kenya inahitaji kushinda michezo miwili dhidi ya Singida Black Stars ya Tanzania ili kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2026/27.

Timu hizo zitakutana katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya mchujo utakaochezwa Jumapili katika Uwanja wa Nyayo, Nairobi.

Tusker inaingia katika mchezo huo ikiwa na morali baada ya kuanza vizuri Ligi Kuu ya Kenya kwa kuifunga Ulinzi Stars mabao 2-0 Jumapili iliyopita na Singida iliitoa timu kutoka Sudani.

Kocha Julien Mette amesema lengo lao kuu ni kufuzu hatua ya makundi kabla ya kuweka malengo mengine katika mashindano hayo.

Mette amesisitiza umuhimu wa kupata ushindi mkubwa nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri kabla ya mchezo wa marudiano nchini Tanzania wiki inayofuata.

Hata hivyo, ameonya wachezaji wake kutowadharau wapinzani hao, akieleza kuwa Singida ni timu yenye ushindani mkubwa.

Tusker huenda ikawakosa baadhi ya wachezaji muhimu kutokana na majeraha na uchovu. Nahodha Abud Omar na Crispine Erambo walikosa mchezo uliopita baada ya kurejea kutoka majukumu ya timu ya taifa, huku Thomas Teka Omenda na Hassan Warsama wakiendelea kuuguza majeraha.

Kwa upande wa Singida Black Stars, timu hiyo imeonesha uwezo mkubwa baada ya kuifunga El-Ghazala ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 10-1 katika raundi ya kwanza.

Ushindi huo unaifanya timu hiyo ya Tanzania kuingia katika mchezo dhidi ya Tusker ikiwa na rekodi nzuri ya ushambuliaji.

Tusker ilifuzu raundi ya pili baada ya kuiondoa Al-Ahli Wad Medani ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-2. Kocha Mette amesema ana imani na ubora wa kikosi chake, huku akisisitiza ushindani wa nafasi ndani ya timu na umuhimu wa kila mchezaji kutoa kiwango cha juu.

Tusker sasa inalenga kupata matokeo mazuri katika mchezo wa nyumbani ili kuongeza nafasi ya kufuzu hatua ya makundi, lakini italazimika kuwa makini dhidi ya Singida ambayo imeonyesha uwezo wa kufunga mabao mengi katika mashindano hayo ya Afrika.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button