Jihan kurejea kesho na taji la kihistoria

DAR ES SALAAM: MREMBO wa Tanzania, Jihan Dimack, anatarajiwa kurejea nchini kesho, Oktoba 17, akiwa na taji la Miss Grand International 2026 alilolitwaa jijini Bangkok, Thailand, na kuiweka Tanzania katika historia ya mashindano ya urembo duniani.
Jihan anarejea nyumbani baada ya kuwa mwanamke wa kwanza kutoka Afrika kutwaa taji hilo tangu mashindano hayo yalipoanzishwa, ushindi unaotajwa kuwa hatua kubwa kwa Tanzania na bara la Afrika katika medani ya urembo wa kimataifa.
Mrembo huyo aliandika historia Oktoba 10 mwaka huu, baada ya kuwashinda washiriki kutoka mataifa mbalimbali katika fainali iliyofanyika Bangkok, ambako aliwashinda washindani waliokuwa wakisaka taji hilo, akiwamo Shyare Andrade wa Ecuador aliyeshika nafasi ya pili.
Ushindi huo ni matokeo ya safari ndefu ya Jihan katika tasnia ya urembo, ambayo ilianza kujulikana zaidi mwaka 2014 aliposhiriki Miss Tanzania na kushika nafasi ya pili, kabla ya kutwaa taji la Miss Universe Tanzania mwaka 2016 na kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Miss Universe yaliyofanyika Ufilipino Januari 2017.
Mwaka huu, Jihan alirejea katika mashindano ya urembo kwa kutwaa taji la Miss Grand Tanzania 2026 Agosti, ushindi uliompa tiketi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa na hatimaye kuibuka mshindi wa jumla.
Mamia ya Watanzania wanatarajiwa kumpokea kuanzia saa 6 mchana Uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.
Hata hivyo, kurejea kwa Jihan kunatarajiwa kuwa fursa ya Watanzania kutambua zaidi mafanikio yake na safari iliyomfikisha katika nafasi ya kuiwakilisha nchi na Afrika katika jukwaa hilo la kimataifa.




