Kwingineko

Simeone amtaka Alvarez aboresha kiwango chake

MADRID: KOCHA wa Atletico Madrid, Diego Simeone, amemtaka mshambuliaji wake Julian Alvarez kuendelea kuimarisha kiwango chake licha ya kushindwa kufunga mabao tangu kuanza kwa msimu huu, huku timu hiyo ikijiandaa kukabiliana na Manchester United katika Ligi ya Mabingwa Ulaya leo.

Manchester United itawasili katika mji mkuu wa Hispania ikiwa na matumaini ya kuendeleza ushindi wake mkubwa wa mechi ya ufunguzi dhidi ya Sabah, wakati Atletico Madrid ilipoteza mchezo wake wa kwanza wa hatua ya ligi dhidi ya Liverpool.

Alvarez, aliyewahi kuichezea Manchester City, amekuwa na mwanzo mgumu wa msimu akiwa Atletico Madrid. Hali hiyo imekuja baada ya mshambuliaji huyo kujaribu kuondoka klabuni hapo wakati wa dirisha la usajili la majira ya kiangazi, akihusishwa na uhamisho kwenda kwa mabingwa wa Hispania Barcelona.

“Ni kweli kwamba mbali na umaliziaji wake, yeye ni mchezaji wa timu, ana uwezo mkubwa wa kuunganisha mchezo, kutoa pasi za mabao na ana vipaji vingi zaidi ya kufunga,” alisema Simeone.

Alvarez aligonga mwamba akiwa kama mchezaji wa akiba katika mchezo dhidi ya Alaves uliopigwa Jumamosi, ambapo Atletico ilishinda na kupanda hadi nafasi ya pili katika msimamo wa La Liga.

Simeone alisema mshambuliaji huyo alionesha kiwango kizuri katika kipindi cha pili cha mchezo huo na kwamba benchi la ufundi linatarajia kuona akiendelea kukua na kufikia kiwango wanachokihitaji.

Ingawa Alvarez alifunga bao akiwa na timu ya taifa ya Argentina katika mechi ya kirafiki dhidi ya Burkina Faso wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa, bado hajafunga katika mechi tano alizoichezea Atletico Madrid.

Atletico Madrid imeibuka na ushindi katika mechi zake nne zilizopita, tofauti na Manchester United ambayo imekuwa na wakati mgumu, ikiwa haijapata ushindi katika mechi nne katika mashindano yote tangu ilipoifunga Sabah.

Kikosi cha kocha Michael Carrick pia kimekumbwa na mwanzo mbaya zaidi wa msimu wa Ligi Kuu England katika kipindi cha miaka 40.

Licha ya fainali ya Ligi ya Mabingwa ya Juni ijayo kupangwa kuchezwa katika uwanja wa Atletico, Metropolitano, Simeone alisema kwa sasa haelekezi mawazo yake kwenye fainali hiyo.

“Ukweli ni kwamba tunapaswa kuzingatia mambo ya kila siku, mchezo mmoja baada ya mwingine,” alisema kocha huyo.

Akizungumzia mchezo dhidi ya Manchester United, Simeone alionya kuwa utakuwa mgumu na wa muda mrefu, hivyo timu yake italazimika kutumia nguvu zake kwa busara ili iweze kushindana kwa kiwango kizuri.

Related Articles

Back to top button