EPL

Haaland: Manchester tunatakiwa kushikamana

MANCHESTER:MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Erling Haaland, amewataka wachezaji wenzake kushikamana na kuendelea kuwa na mtazamo chanya katika kipindi hiki cha sintofahamu kinachokikabili klabu hiyo, baada ya kupatikana na hatia ya kukiuka zaidi ya vipengele 100 vya kanuni za kifedha za Ligi Kuu England.

Manchester City inakabiliwa na uwezekano wa kuadhibiwa kwa kupunguziwa alama nyingi au hata kufukuzwa katika Ligi Kuu England, kufuatia uamuzi wa tume huru iliyochunguza tuhuma dhidi ya klabu hiyo.

Tume hiyo ilibaini kuwa kati ya mwaka 2009 na 2018, klabu hiyo ilitumia mikataba ya kibiashara iliyotajwa kuwa ya kujifanya ili kuongeza mapato na kupunguza gharama kwa zaidi ya pauni milioni 900, sawa na takribani dola bilioni 1.2 za Marekani.

Haaland, ambaye alijiunga na Manchester City mwaka 2022, hakuwapo klabuni hapo wakati wa kipindi kinachohusishwa na ukiukaji huo. Hata hivyo, kikosi cha sasa kinaweza kuathiriwa na adhabu yoyote itakayotolewa.

Akizungumza kupitia tovuti rasmi ya klabu hiyo, Haaland amesisitiza umuhimu wa wachezaji kuendelea kuunga mkono kila mmoja, kuangalia mbele na kuelekeza nguvu zao katika ushindi uwanjani licha ya changamoto zinazoikabili timu hiyo.

“Tunapaswa kubaki na mtazamo chanya, kuangalia mbele na kujaribu kushinda mechi za soka. Tunapaswa pia kufurahia hali tuliyopo na kushinda mchezo,” alisema Haaland.

Aliongeza: “Tunapaswa kushikamana na kuendelea kuonyeshana upendo.

“Kwa hiyo, tushikamane, tufurahie safari yetu na tuendelee kutabasamu.”

Manchester City, ambayo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu England, inatarajiwa kurejea dimbani Jumapili kwa mara ya kwanza tangu taarifa ya kupatikana na hatia ilipotangazwa, itakapokutana na Liverpool.

Haaland alisaini mkataba mpya na Manchester City mwaka jana utakaomuweka klabuni hapo hadi mwaka 2034. Hata hivyo, mustakabali wake unaweza kuathiriwa na uzito wa adhabu itakayotolewa dhidi ya klabu hiyo.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button