
LAGOS: MUIMBAJI wa nyimbo za Injili kutoka Nigeria, Osinachi Okoro, maarufu kama Sinach, amefunguka kuhusu safari yake ya ndoa na umama, akieleza namna alivyopitia kipindi cha kusubiri kwa miaka kadhaa kabla ya kupata mtoto wake wa kwanza.
Sinach amesema aliolewa mwaka 2014 na Mchungaji Joseph Egbu akiwa na umri wa miaka 41, lakini hakupata mtoto mara moja, hali iliyomfanya asubiri kwa takribani miaka mitano kabla ya kujaliwa mtoto wake wa kwanza.
Amesema katika kipindi hicho alikabiliwa na maswali na shinikizo kutoka kwa baadhi ya watu waliotaka kujua lini angepata mtoto, lakini hakuruhusu hali hiyo kumzuia kuendelea na maisha yake.

Badala yake, Sinach amesema aliendelea kumtumikia Mungu, kuandika na kuimba nyimbo, pamoja na kujenga ndoa yake huku akiendelea kuwa na matumaini.
Mwaka 2019, akiwa na umri wa miaka 46, Sinach alijaliwa kupata mtoto wake wa kwanza, binti aitwaye Rhoda, ambaye amekuwa sehemu muhimu ya maisha yake.
Akizungumzia uzoefu huo, Sinach amewatia moyo watu wanaopitia vipindi vya kusubiri katika maisha yao kutoruhusu kuchelewa kwa jambo fulani kuwaondolea furaha, amani na imani.
Amesema kila mtu ana safari yake na wakati wake, hivyo kipindi cha kusubiri hakipaswi kuchukuliwa kama mwisho wa matumaini.
“Siyo kuhusu lini mambo yanatokea. Ni kuhusu nani unayemtumaini unaposubiri,” amesema Sinach.




