Mastaa

Harmonize atamba na penzi jipya

DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’, amemtambulisha mpenzi wake mpya kupitia ukurasa wake wa mtandao ya kijamii, miezi kadhaa baada ya kuvunjika kwa uhusiano wake na Kajala Masanja.

Harmonize amecha[pisha picha inayomuonesha akiwa na mpenzi huyo mpya na kuambatanisha ujumbe mfupi uliosomeka “Great time”, hatua iliyozua mjadala miongoni mwa mashabiki na wadau wa burudani.

Uhusiano wa Harmonize na Kajala umekuwa ukifuatiliwa kwa karibu na mashabiki kutokana na historia yao ya mapenzi, huku wawili hao wakirudiana na kutengana mara kadhaa.

Baada ya Harmonize kumtambulisha mpenzi wake mpya, baadhi ya wadau kwenye mitandao ya kijamii walitoa maoni tofauti kuhusu hatua hiyo, huku mmoja akidai kuwa kurejea kwa Harmonize na Kajala hapo awali huenda hakukuwa na msingi wa mapenzi pekee.

Mdau huyo alidai kuwa Harmonize huenda alikuwa na nia ya kulipiza kisasi kutokana na namna uhusiano wao ulivyovunjika awali, akieleza kuwa msanii huyo aliumia baada ya kuachwa na Kajala.

Hata hivyo, madai hayo hayajaungwa mkono na ushahidi wa wazi kutoka kwa Harmonize au Kajala, hivyo yanaendelea kubaki kuwa maoni na hisia za mdau huyo kwenye mitandao ya kijamii.

Mdau huyo pia alikosoa kitendo cha Harmonize kumtambulisha mpenzi wake mpya wakati Kajala akidaiwa kuwa anapitia kipindi kigumu, akisema msanii huyo alipaswa kuzingatia hali hiyo kabla ya kuweka wazi uhusiano wake mpya.

Kwa upande mwingine, Harmonize katika ujumbe wake hakutoa maelezo kuhusu historia ya uhusiano wake mpya wala kuhusisha hatua hiyo na Kajala, bali aliambatanisha picha hiyo na ujumbe mfupi wa kuonesha kufurahia muda aliokuwa nao.

Hatua hiyo imeendelea kuongeza mjadala kwenye mitandao ya kijamii, huku mashabiki wakisubiri kuona kama Harmonize atatoa maelezo zaidi kuhusu uhusiano wake mpya.

Related Articles

Back to top button