Liverpool yaingia dili nono na Turkish Airlines

LIVERPOOL: KLABU ya Liverpool imeingia mkataba wa mdhamini mkuu mpya wa jezi na Kampuni ya Turkish Airlines wenye thamani ya Pauni milioni 60 kwa mwaka.
Mkataba huo wa miaka mitano utakaoingiza zaidi ya Pauni milioni 300, utaanza kutumika rasmi msimu wa 2027-28.
Dili hilo linawaondoa Standard Chartered waliodumu na Liverpool tangu mwaka 2010 na sasa jezi za timu za wanaume, wanawake na akademi kifuani zitaandikwa Turkish Airlines.
Standard Chartered ilikuwa ikitoa Pauni milioni 50 lakini dili la sasa linaifanya Liverpool kufungana kileleni na Machester United kwa kupokea vitita vikubwa vya udhamini kwa mwaka Ligi Kuu ya England.
Manchester inadhaminiwa na Qualcomm Snapdragon walioingia nao mkataba mwaka 2024.
“Hii ni taarifa muhimu sana kwetu, tunafurahi kuwakaribisha Turkish Airlines kama washirika wetu wakuu wa klabu kuanzia Juni 2027,” alisema Ofisa Mkuu wa Biashara wa Liverpool, Ben Latty na kuongeza:
“Sehemu ya mbele ya jezi ya Liverpool ina nafasi ya kipekee katika historia ya klabu yetu. Turkish Airlines ni shirika linalotambulika na lenye mtandao mpana kimataifa; tutajenga ushirikiano, uhusiano imara, juu ya misingi imara iliyopo kutokana na kumbukumbu za kipekee za mwaka 2005 (ubingwa wa Uefa dhidi ya AC Milan, Istanbul).”
Liverpool sasa inakuwa klabu ya nne England kudhaminiwa na shirika la ndege baada ya Arsenal wenye Fly Emirates, Manchester City (Etihad Airways) na Hull City (Corendon Airlines).
Aidha, taarifa zinaeleza pengine jezi ya Liverpool msimu ujao itakuwa na mabadiliko zaidi kwani mdhamini wa begani, Kampuni ya Expedia pia inamaliza mkataba wake mwisho wa msimu huu.
Expedia iliongeza mkataba na Liverpool mwaka 2023 uliofikia thamani kati ya Pauni milioni 9 mpaka 12 kwa mwaka.




