Nyumbani

Massanza, Pablo watozwa mamilioni ya fedha

DAR ES SALAAM: KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewatoza faini maofisa wawili wa Singida Black Stars Hussein Massanza na Pablo Almasi kila mmoja sh milioni 10 huku Polisi Tanzania nayo ikitozwa kiwango hicho kwa makosa mbalimbali.

Massanza, ambaye ni Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, ametozwa faini ya Sh milioni 10 kwa kumshutumu na kumtukana mwamuzi wa kati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba SC kupitia chapisho la mtandaoni.

Kwa mujibu wa taarifa ya TPLB, Massanza amekiuka Kanuni ya 49:3 na 49:4 kuhusu udhibiti kwa maofisa habari wa klabu, huku adhabu hiyo ikitolewa chini ya Kanuni ya 49:7.

Pablo Almasi, ambaye pia ni Ofisa wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, naye ametozwa faini ya Sh milioni 10 kwa kusambaza machapisho kwenye ukurasa wake wa Instagram yaliyokuwa na maudhui ya kumkashifu mwamuzi wa mchezo huo.

Aidha, TPLB imesema Almasi alikebehi teknolojia ya Football Video Support (FVS) katika mchezo wa Yanga dhidi ya Coastal Union, jambo lililosababisha kukiuka Kanuni ya 49:4 na 49:5. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 49:7.

Katika hatua nyingine, Polisi Tanzania imepigwa faini ya Sh milioni 10 kwa kosa la kumjumuisha mchezaji mmoja pekee kutoka timu yake ya vijana kwenye orodha ya wachezaji 21 kwa ajili ya mchezo dhidi ya Singida Black Stars, uliomalizika kwa Singida kushinda 4-2.

Klabu hiyo imekiuka matakwa ya Kanuni ya 17:6(6.2) kuhusu taratibu za mchezo, na adhabu imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62.

Kamati pia imetoa maonyo makali kwa Namungo FC na Geita Gold kutokana na ukiukaji wa taratibu za maandalizi ya michezo.

Namungo imepewa onyo kali kwa kuchelewa kuwasili Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam, kuelekea mchezo dhidi ya JKT Tanzania, uliochezwa Agosti 29, 2026.
Klabu hiyo iliwasili saa 1:55 usiku badala ya saa 1:30 usiku.

Geita Gold nayo imepewa onyo kali baada ya maofisa wake kuchelewa kwa dakika 15 kufika kwenye kikao cha kitaalamu cha maandalizi na uratibu wa mchezo dhidi ya Simba SC.

Mbali na onyo hilo, Geita Gold imetozwa faini ya Sh milioni 10 kwa kuwakilishwa na maofisa wawili pekee kwenye kikao hicho, kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17.29(2.1.1).

Katika mchezo wa Kagera Sugar dhidi ya Azam FC uliomalizika kwa Azam kushinda 2-0, TPLB imefuta adhabu ya kadi nyekundu aliyooneshwa mchezaji wa Azam, Gibril Sillah, baada ya kujiridhisha kupitia picha jongeo na taarifa za wataalamu kuwa hakustahili adhabu hiyo.

Uamuzi huo umefanyika kwa kuzingatia Kanuni ya 12:8 kuhusu usimamizi wa ligi.
Hata hivyo, mwamuzi wa akiba wa mchezo huo, Greyson Buchard wa Kagera Sugar, amepewa onyo kali kwa kosa la kuonesha mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyotokana na kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu.

TPLB imesema adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 43:1(1.8) kuhusu udhibiti kwa waamuzi.
Kamati imezikumbusha klabu zote kuzingatia kikamilifu kanuni za ligi ili kuepuka adhabu zinazotokana na ukiukaji wa taratibu za mashindano.

Related Articles

Back to top button