Michezo Mingine

Kriketi Tanzania yaichapa Namibia

DAR ES SALAAM:TANZANIA imepata ushindi wa mikimbio 25 dhidi ya Namibia katika Mashindano ya Kufuzu Kombe la Dunia la ICC T20 kwa Wanawake U-19 Kanda ya Afrika, yanayoendelea katika viwanja vya Chuo Kikuu jijini Dar es Salaam.

Tanzania ilimaliza zamu yake ya kupiga mpira ikiwa imefunga mikimbio 100 huku wachezaji wake wanane wakiondolewa (100/8). Katika zamu ya Namibia, Tanzania ilionesha kiwango bora katika kurusha mpira, na hatimaye kuiondoa Namibia ikiwa imefunga mikimbio 75 baada ya kucheza mipira 95.

Mchezaji wa Tanzania Lightness Eliud ametajwa kuwa mchezaji bora wa mechi, baada ya kuonesha kiwango bora katika upigaji na urushaji wa mpira.

Eliud alifunga mikimbio 11 kwa mipira 12, kabla ya kung’ara zaidi katika urushaji wa mpira kwa kuwaondoa wachezaji wanne wa Namibia, huku akiruhusu mikimbio 27 katika seti nne za mipira.

Mchango wake ulikuwa muhimu katika kuisaidia Tanzania kupata ushindi wa mikimbio 25 dhidi ya Namibia.

Ushindi huo umeiwezesha Tanzania kufuzu kucheza mchezo wa kuwania nafasi ya tano katika mashindano hayo.

Related Articles

Back to top button