Michezo MingineRiadha

‘SUPER-SHOES’>>> Viatu vinavyomsaidia mwanariadha kushinda

REKODI za dunia za marathoni zimekuwa zikiporomoka kwa haraka katika mbio za wanaume na wanawake hivi karibuni, lakini gumzo kubwa limekuwa katika viatu vinavyotumiwa na wanariadha hao vya ‘super- shoes’.

Viatu hivyo ndivyo vinaelezwa kuwa vinachangia kwa wanariadha kuvunja rekodi mbalimbali zikiwemo zile za dunia katika kipindi cha muda mfupi.

Huko nyuma rekodi za dunia zilikuwa zinadumu kwa muda mrefu tangu zivunjwe tofauti na sasa, ambapo zimekuwa zikivunjwa mara kwa mara.

REKODI ZA ZAMANI
Mfano rekodi ya dunia ya nguli wa riadha nchini, Filbert Bayi ya umbali wa meta 1,500
aliyoiweka mwaka 1974 katika Michezo ya Jumuiya ya Madola huko Christchurch, New Zealand alidumu nayo kwa miaka mitano kabla ya kuja kuvunjwa na Sebastian Coe.

Wakati Bayi alidumu na rekodi yake hiyo ya dunia kwa miaka mitano, alidumu na rekodi ya Jumuiya ya Madola kwa zaidi ya miaka 40 hadi ilipovunjwa mwaka jana.

Wapo wanariadha wengi waliodumu na rekodi zao kwa muda mrefu miaka ya nyuma, lakini sasa imekuwa tofauti, kwani rekodi zimekuwa zikivunjwa kila mara.

REKODI ZA SASA
Mwanariadha wa Ethiopia, Tigst Assefa alivunja rekodi ya dunia ya mbio za marathoni kwa wanawake mjini Berlin Septemba 24, 2023 baada ya kumaliza mbio hiyo kwa saa 2:11:53, ikiwa ni dakika mbili na sekunde 11 kutoka kwa rekodi iliyowekwa na Brigid Kosgei wa Kenya huko Chicago mwaka 2019.

Assefa, mtaalamu wa zamani wa mbio za meta 800, alianza kukimbia marathoni Machi mwaka 2022 na alikuwa amevalia kiatu cha Adidasi chenye thamani ya Pauni 400
(sawa na Sh milioni 1.2) aina ya Adizero Adios Pro Evo 1.

MAMBO ZAIDI
Mkimbiaji wa mbio ndefu wa Kenya, Kelvin Kiptum alivuka mstari wa kumaliza mbio akiwa
ameweka rekodi ya dunia katika Chicago Marathon hivi karibuni, huku akiwa amevalia viatu vinavyojulikana kama Nike Dev 163. Nike walithibitisha kuwa ni viatu vya Alphafly 3.

Kiptum alimaliza mbio hizo akitumia saa 2:00:35, akiivunjilia mbali rekodi ya Mkenya mwenzake, Eliud Kipchoge aliyoiweka kwa sekunde 34. Ni mafanikio makubwa kwa mtu kushindana katika marathoni yake ya tatu, sasa ameboresha moja kati ya muda wa kasi zaidi katika historia ya mbio.

Aliweka rekodi yake bora binafsi ya muda wa saa 2:01:53 akianza kukimbia marathoni huko Valencia Desemba 2022  ikiwa ni muda wa sita kwa kasi zaidi katika historia na
kuuboresha muda huo kwa sekunde 28 wakati aliposhinda London Marathoni mwaka
huu, ikiwa ni muda wa tatu kwa kasi zaidi kuwahi kutokea.

Chicago Marathon kwa wanawake mshindi alikuwa Sifan Hassan, aliyeweka rekodi ya njia, ambaye naye pia alivaa viatu vya Alphafly 3s, ambavyo inaelezwa kuwa vilimsaidia kufanya vizuri.

NI VIATU GANI
Swali kubwa kwa sasa ni hivi ‘super-shoes’ ni viatu gani, na wanariadha kama Kiptum na
Assefa wakivaa vinawasaidia kufanya vizuri?

Shirikisho la Riadha la Dunia (WA) linajaribu kutoa njia kutumika kwa teknolojia katika
miaka ya hivi karibuni na WA wamefanya marekebisho katika kanuni na sheria zake Januari
mwaka 2022 ili kuruhusu viatu hivyo kutumika.

Marekebisho hayo iliyatoa katika hati yenye kurasa 18, ambayo inaelezea kuwa viatu havitaanza kutumika katika mashindano hadi pale vitakapokuwa vinapatikana kwa urahisi ili kumuwezesha mwanariadha yeyote kuweza kuvitumia.

Pia mahitaji ya kiufundi lazima yawepo katika suala zima la wembamba au udogo wa soli.
WA inasema viatu vya Alphafly 3s wameviidhinisha, hivyo viko katika orodha yao ya viatu vinavyokubaliwa vyenye mahitaji ya kiufundi.

Viatu vya Nike Alphafly 3, ambavyo vimeboreshwa katika soli yake vimekubaliwa kutumika,
ambapo Nike imesema itavitoa rasmi mwakani kwa ajili ya matumizi.

Hata hivyo, Nike bado haijaweka hadharani uzito wa viatu hivyo vya Alphafly 3s, lakini vina bati ngumu au vijiti vilivyopachikwa katikati ya soli, kwa kawaida hutengenezwa kwa kaboni, ili kusaidia kiatu kushikilia umbo lake na kina umbo lililopinda ili kusaidia kumsogeza mbele mkimbiaji.

ABADILI MCHEZO
Mwanariadha Kipchoge amebadili kabisa mchezo wa riadha hasa katika mbio ndefu.

Alishinda medali ya dhahabu katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2016 na alirudia mwaka 2020, wakati akiweka rekodi ya dunia mwaka 2018 – ikiwa ni kasi zaidi kwa sekunde 18 ya ile ya awali iliyowekwa miaka minne iliyopita.

Kipchoge aliweka historia mwaka 2019 wakati alipokuwa mtu wa kwanza kushinda katika marathoni chini ya saa mbili akitumia saa 1:59:40, huko Vienna, Austria.

Hata hivyo, muda huo hakutambuliwa kama rekodi rasmi ya dunia ya marathoni kwa sababu hayakuwa mashindano ya wazi, baada ya Kipchoge kutumia wasaidizi 41 pamoja na baiskeli iliyokuwa ikitoa unyevunyevu wakati wote.

Related Articles

Back to top button