Filamu

Onesho la filamu ya mazingira kuoneshwa Tambaza

DAR ES SALAAM: FILAMU ya makala Guardians of the Peak, inayolenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira ya Mlima Kilimanjaro na kuongeza uelewa kuhusu vivutio mbalimbali vya utalii nchini, kwa kushirikiana na Lions Club of Humanity Dar es Salaam, wameandaa onesho maalumu la filamu hiyo kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tambaza jijini Dar es Salaam.

Onesho hilo lililenga kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira, changamoto zinazoikabili baadhi ya maeneo ya asili pamoja na wajibu wa jamii katika kulinda rasilimali hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kupitia filamu hiyo, wanafunzi walipata fursa ya kujifunza kuhusu mazingira na umuhimu wa kuyatunza, huku wakihamasishwa kuwa sehemu ya juhudi za uhifadhi kuanzia katika jamii zao.

Mbali na kutazama filamu hiyo, wanafunzi walishiriki katika mijadala na vipindi vya elimu ya mazingira, ambapo walipata nafasi ya kujadili changamoto mbalimbali zinazohusiana na uharibifu wa mazingira na namna vijana wanavyoweza kushiriki katika kuzitatua.

Wanafunzi pia walipata fursa ya kuwasilisha bunifu na maandiko mbalimbali yanayohusu utunzaji na uhifadhi wa mazingira, hatua ambayo imeelezwa kuwa muhimu katika kuwapa vijana nafasi ya kutumia maarifa na ubunifu wao kutafuta suluhisho la changamoto za kimazingira.

Waandaaji wamesema ushirikishwaji wa wanafunzi katika shughuli kama hizo ni muhimu kwa sababu vijana ni miongoni mwa wadau muhimu katika kuhakikisha elimu ya uhifadhi wa mazingira inaendelea kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Tukio hilo pia liliambatana na zoezi la upandaji miti, ikiwa ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuongeza uoto wa asili na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

Kwa kuunganisha elimu ya mazingira, filamu, ubunifu wa wanafunzi na vitendo vya uhifadhi kama upandaji miti, waandaaji wamelenga kuwafanya vijana kuelewa kuwa jukumu la kulinda mazingira ni la kila mmoja na linahitaji ushirikiano wa jamii nzima.

Guardians of the Peak inaendelea kuwa sehemu ya juhudi za kutumia sanaa na filamu kama nyenzo ya kutoa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira, huku ikichochea uelewa kuhusu umuhimu wa kulinda maeneo ya asili na vivutio vya utalii nchini.

Related Articles

Back to top button