Matola: Coastal Union haitakuwa mechi rahisi kwa Simba

DAR ES SALAAM: KOCHA Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, amesema mchezo dhidi ya Coastal Union si mchezo rahisi, licha ya wapinzani kutokuwa na matokeo mazuri katika michezo ya mwanzo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Matola amesema Coastal Union imekuwa ikicheza vizuri na ina kikosi chenye ushindani, jambo linalomfanya kutarajia mchezo mgumu utakaohitaji umakini mkubwa kutoka kwa wachezaji wake.
“Naamini haitakuwa mechi rahisi kwa sababu siku zote Simba na Coastal Union hazina mechi rahisi. Ukiangalia, wenzetu wamekuwa hawapati matokeo mazuri, lakini wamekuwa wakicheza vizuri na wana timu yenye ushindani. Hilo linanifanya niamini kuwa itakuwa mechi ngumu kesho,” amesema Matola.
Amesema pamoja na ugumu unaotarajiwa, Simba imejiandaa vizuri kuhakikisha inapata alama tatu muhimu katika mchezo huo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Jenerali Isamuhyo.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Kocha wa Coastal Union, Fikiri Elias, amesema wameufanyia kazi mfumo wa Simba na namna wanavyocheza, hususan kutumia mashambulizi ya haraka na udhibiti wa eneo la kiungo.

“Tunafahamu ubora na ushindani ambao Simba wamekuwa wakiuleta katika mchezo. Sote tumejiandaa kuwakabili. Tunafahamu Simba wanacheza mpira wa kushambulia haraka, lakini pia wanajua kumiliki katika eneo la katikati, hivyo tumejipanga kwenye hilo.
“Tunatambua wanakuwa hatari kidogo wakati timu pinzani inapopata mpira kwenye njia. Sote tumeweka mipango yetu na muda wetu wa kukabiliana nao, lengo likiwa ni kupata matokeo mazuri katika mchezo wa kesho,” amesema Elias.




