Rema atangaza onesho nchini Rwanda

NIGERIA: Msanii wa Afrobeats kutoka Nigeria, Rema, anatarajiwa kuwa msanii mkuu katika tamasha la Kwita Izina Concert 2026, tamasha litakalofanyika katika ukumbi wa BK Arena jijini Kigali, Rwanda, Septemba 5, 2026.
Rema atapanda jukwaani siku moja baada ya kufanyika kwa hafla ya 21 ya Kwita Izina Gorilla Naming Ceremony, inayotarajiwa kufanyika Septemba 4 katika eneo la Kinigi, Musanze District, ambapo gorilla waliozaliwa karibuni watapewa majina.
Msanii huyo anayefahamika kwa ngoma zake kubwa ikiwemo ‘Calm Down’, amekuwa miongoni mwa wasanii wa Afrika wenye ushawishi mkubwa kimataifa, huku muziki wake ukiendelea kufanya vizuri katika masoko mbalimbali duniani.

Katika tamasha hilo, Rema ataungana na wasanii wengine kutoka Rwanda na ukanda wa Afrika Mashariki, akiwemo Kivumbi King, huku waandaaji wakitarajiwa kutangaza wasanii wengine watakaoshiriki katika tukio hilo.
Kwa mujibu wa Rwanda Development Board (RDB), tamasha hilo ni sehemu ya sherehe za Kwita Izina zinazolenga kuunganisha uhifadhi wa mazingira, utalii, utamaduni na burudani, huku ujio wa Rema ukitarajiwa kuvutia mashabiki kutoka Rwanda na nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.
Ujio wa Rema Kigali unatarajiwa kuongeza mvuto wa sherehe za mwaka huu na kuifanya BK Arena kuwa kitovu cha burudani katika ukanda huo, huku mashabiki wakisubiri kwa hamu kuona moja ya mastaa wakubwa wa Afrobeats akifanya onyesho lake nchini Rwanda.




