Afrika Mashariki

Tanzania, Kenya na Uganda zatakiwa kufika nusu fainali Afcon 2027

NAIROBI: TANZANIA, Kenya na Uganda zimepewa jukumu la kuhakikisha zinafanya vizuri katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, ambazo zitaandaliwa kwa pamoja na mataifa hayo matatu ya Afrika Mashariki.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya AFCON 2027 nchini Kenya (LOC), Nicholas Musonye, amesema matarajio yao si kuandaa tu mashindano hayo, bali pia kuhakikisha angalau moja kati ya timu za Harambee Stars ya Kenya, Taifa Stars ya Tanzania na Cranes ya Uganda inafika hatua ya nusu fainali.

Musonye amesema wanataka mataifa hayo matatu yawe na timu imara zitakazoweza kushindana na mataifa mengine makubwa barani Afrika.

“Tunataka Harambee Stars yetu, Taifa Stars ya Tanzania na Cranes ya Uganda ziwe imara. Kati ya timu nne zitakazofika nusu fainali, lazima tuwe na timu moja au mbili,” amesema Musonye.

Amesema lengo lao ni kuandaa mashindano ambayo nchi mwenyeji zitashiriki kwa ushindani na kulenga kutwaa ubingwa, badala ya kushiriki kwa ajili ya kujaza idadi.

“Tunataka kuandaa mashindano na kushindana ili kushinda, siyo kushiriki tu,” amesema.

Mbali na mafanikio ya uwanjani, Musonye amesema AFCON 2027 inapaswa kuwa chanzo cha fursa kubwa za kiuchumi kwa wananchi wa Afrika Mashariki.

Amesema kamati ya maandalizi imeandaa mfumo utakaowawezesha wafanyabiashara na kampuni za ndani kushiriki katika mchakato wa zabuni na utoaji wa huduma mbalimbali zinazohitajika wakati wa mashindano.

“Tuna fursa kubwa za biashara kwa watu wetu. Tumeandaa mfumo ambao tunataka watu wetu washiriki katika mchakato wa manunuzi ya shughuli tutakazozifanya,” amesema.

Kwa mujibu wa Musonye, mahitaji yatakuwa katika maeneo mbalimbali, huku biashara ya bidhaa za mashindano, huduma na biashara ndogo ndogo zikitarajiwa kunufaisha wafanyabiashara wengi.

Amesisitiza kuwa sekta isiyo rasmi pamoja na wananchi wa kawaida, wanapaswa kupata manufaa ya moja kwa moja kutokana na mashindano hayo.

“Hatukutaki kuwa na AFCON halafu watu waondoke bila kupata chochote. Tunataka wafanyabiashara wetu, wananchi wanufaike na tukio hili.” Amesema Musonye.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button