Venus apewa nafasi ya kipekee kushiriki US Open

NEW YORK: Bingwa wa zamani wa US Open, Venus Williams, amepewa nafasi ya kipekee ‘wild card’ ya kushiriki moja kwa moja kwenye mashindano ya US Open ya mwaka huu.
Venus, mwenye umri wa miaka 46, ni miongoni mwa wachezaji waliopata nafasi hiyo kutoka Shirikisho la Tenisi la Marekani (USTA) kuelekea mashindano hayo yatakayofanyika New York kuanzia Agosti 30 hadi Septemba 13.
Venus amewahi kushinda mataji mawili ya US Open, mwaka 2000 na 2001, pamoja na mataji matano ya Wimbledon.
Hata hivyo, amekuwa akipitia kipindi kigumu katika mchezo wa tenisi, baada ya kupoteza mechi zake 14 zilizopita za WTA singles, kuanzia Julai 2025.
Miongoni mwa wachezaji wengine wa kike waliopata ‘wild cards’ ni pamoja na Sloane Stephens, bingwa wa US Open mwaka 2017, Carol Young Suh Lee, Reese Brantmeier na Thea Frodin mwenye umri wa miaka 17.
Kwa upande wa wanaume, nyota wa Ufaransa Gaël Monfils nay ni mnufaika kwa ‘wild card’ huku akitarajiwa kutimiza miaka 40 mwezi Septemba na ametangaza kustaafu kucheza tenisi mwishoni mwa msimu huu.
Kwa upande mwingine, nafasi moja ya ‘wild card’ bado imeachwa wazi katika droo ya wanawake, hali inayozua uwezekano wa dada wa Venus, Serena Williams naye kupewa nafasi ya kushiriki mashindano hayo.
Serena mwenye umri wa miaka 44 ni bingwa mara sita wa US Open na mshindi wa mataji 23 ya Grand Slam.
Serena alirejea kwenye mashindano ya Wimbledon mwaka huu baada ya kutoshiriki kwenye droo ya mchzaji mmoja mmoja ya Grand Slam tangu mashindano ya US Open ya mwaka 2022.
Jumatatu iliyopita, Venus na Serena Williams walicheza pamoja katika mashindano ya Cincinnati Open katika mchezo wa wachezaji wawili wawili ‘doubles’, ikiwa ni mara yao ya kwanza kucheza pamoja kwa miaka minne, lakini walipoteza mchezo huo.




