BASATA, BoT na Bodi ya filamu kutoa elimu ya fedha kwa wasanii

DAR ES SALAAM: BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA), kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na Bodi ya Filamu Tanzania, limeanza mikakati ya kuimarisha utoaji wa elimu ya fedha kwa wasanii na wananchi kwa ujumla ili kuongeza uelewa kuhusu masuala ya kifedha na uzingatiaji wa sheria zinazohusiana na huduma ndogo za fedha.
Hatua hiyo imejadiliwa katika kikao kilichomshirikisha Kaimu Katibu Mtendaji wa BASATA, Edward Buganga, pamoja na viongozi kutoka BoT, Bodi ya Filamu Tanzania na Umoja wa Machifu Tanzania, kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho, Buganga amesema ushirikiano huo unalenga kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wasanii na wadau wa sekta ya sanaa ili kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa na mamlaka husika.
Katika majadiliano hayo, washiriki wamesisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa wananchi, hususan wasanii na waigizaji, kuhusu matumizi sahihi ya huduma ndogo za fedha pamoja na wajibu wao katika kufuata taratibu za kifedha zinazotambuliwa kisheria.
Kwa upande wake, Benki Kuu ya Tanzania imeeleza kuwa shughuli za ukopeshaji zinapaswa kufanywa na watu binafsi au taasisi zilizopewa leseni rasmi, huku ikiwataka wasanii na wananchi kuwa waangalifu na kujiepusha na mifumo ya ukusanyaji fedha kupitia vikundi au ‘upatu’ usiosajiliwa, ambayo inaweza kuhatarisha usalama wa fedha zao.
Aidha, BoT imetoa elimu kuhusu umuhimu wa kutunza noti na sarafu za Tanzania, ikisisitiza kuwa fedha ni tunu ya Taifa inayopaswa kuhifadhiwa kwa uangalifu.
Wasanii na wananchi walikumbushwa kuepuka vitendo vinavyosababisha uharibifu wa noti na sarafu, ikiwemo kuzikunja ovyo, kuziweka katika mazingira yenye unyevunyevu au uchafu, pamoja na kuzitumia kwa namna inayoweza kuziharibu wakati wa sherehe na matukio mbalimbali ya kijamii.
BASATA imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na BoT pamoja na wadau wengine kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wasanii wengi zaidi nchini, hatua itakayosaidia kuongeza uelewa wa masuala ya fedha, kuimarisha uwajibikaji na kuchangia katika utunzaji wa fedha za Tanzania kama sehemu ya urithi na tunu ya Taifa.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuwa chachu ya kuwajengea wasanii uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha na kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia misingi ya sheria na usimamizi bora wa rasilimali fedha.




