Lomalisa aibukia Bandari

DAR ES SALAAM: BEKI wa zamani wa Yanga na Azam, Joyce Lomalisa, amejiunga na Bandari FC inayoshiriki Championship msimu huu, ikiwa ni hatua ya timu hiyo kuimarisha kikosi chake katika harakati za kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara.
Lomalisa, ambaye anacheza nafasi ya beki wa kushoto, amesaini kujiunga na Bandari baada ya kumalizana na klabu ya Academica Petroleos do Lobito ya Angola, alikokuwa akicheza kabla ya kurejea nchini.
Usajili wa beki huyo mwenye uzoefu wa kucheza katika ushindani wa juu unatarajiwa kuongeza ubora na uzoefu kwenye kikosi cha Bandari, ambacho kimepanda kutoka First League na sasa kinajiandaa kwa msimu mpya wa Championship.
Bandari, ambayo ina historia kubwa katika soka la Tanzania, imeweka wazi azma yake ya kutumia msimu huu kama daraja la kurejea Ligi Kuu, huku ikifanya usajili wa wachezaji wenye uzoefu ili kujenga kikosi chenye ushindani.
Timu hiyo ina historia ya kuzalisha na kutoa wachezaji waliokuja kuwa majina makubwa katika soka la Tanzania. Miongoni mwao ni mshambuliaji Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, ambaye bado anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mmachinga aliweka rekodi hiyo baada ya kufunga mabao 26 katika msimu mmoja, rekodi ambayo hadi sasa haijavunjwa na mshambuliaji mwingine katika historia ya ligi hiyo.




