‘Baleke ni mtu na nusu’
MENEJA wa timu ya Yanga, Walter Harrison amemtaka mshambuliaji wa timu hiyo, Jean Baleke kujituma na kupambana zaidi mazoezini kwa lengo ya kumshawishi kocha Miguel Gamondi.
Walter amesema mchezaji yoyote anahitaji kucheza lakini sio rahisi kocha kuibadili timu ya ushindi na ndicho kinachotokea kwa Jean Baleke na nyota wengine wa Yanga.
“Kuna mashindano mengi moja kwa moja anaweza kupata nafasi, ninaimani na uwezo wa Baleke, atakuja kuonyesha kiwango bora na anajua kufunga.
Kikubwa kuendelea kupambana pale anapokuwa kwenye uwanja wa mazoezi na anapopata nafasi ya kucheza katika mechi kumshawishi kocha,” amesema Walter.
Ameongeza kuwa licha ya Baleke kutopata nafasi mara kwa mara nyota huyo amekuwa na hamasa kubwa kwa wachezaji wenzake waliopo uwanjani.
“Tunakumbuka mechi yetu ya marudiano dhidi ya CBE SA tuliocheza Zanzibar, hakuwa kwenye mipango ya mchezo huo lakini dakika 45 ya kipindi cha kwanza aliingia vyumba vya kubadilishia kuongea na kuwakumbusha wenzake,” amesena meneja huyo.
Hivi karibuni Kocha Gamondi amesema inampa ugumu kumchezesha mshambuliaji Jean Baleke kwa sababu itampasa amtoe Clement Mzize au Prince Dube.
Amesema anajua uwezo wa Baleke lakini kwa sasa Prince Dube na Clement Mzize wanakidhi mahitaji yake katika mfumo wake kuliko Baleke ambaye bado ni mgeni na anahitaji kuujua mfumo, na sio kitu rahisi.