Priscy ajiita ‘Mrs Free Jux’

DAR ES SALAAM: MKE wa msanii wa Bongo Fleva, Juma Jux, Priscilla, ameamua kuuchukulia kwa utani ujumbe wa mashabiki waliokuwa wakitumia kauli ya “Free Jux” kwenye machapisho yake ya hivi karibuni.
Kauli hiyo, ambayo kwa tafsiri rahisi ina maana ya “Mwachieni Jux”, imekuwa ikijitokeza mara kwa mara katika maoni ya mashabiki kila Priscilla anapoweka picha au video zinazomhusu yeye na mumewe.
Badala ya kukasirika, Priscilla ameamua kugeuza utani huo kuwa sehemu ya utambulisho wake, baada ya kubadilisha wasifu wake (bio) na kuongeza maneno “Mrs Free Jux.”
Hatua hiyo imezua gumzo miongoni mwa mashabiki, huku wengi wakiona kuwa Priscilla ameamua kuupokea ujumbe huo kwa mtazamo wa kipekee na wa utani.
Kwa sasa, Jux na Priscilla wanaendelea kusalia nchini Nigeria, ambako wameonekana wakihudhuria sherehe na matukio mbalimbali.
Katika baadhi ya video zinazosambaa mitandaoni, Jux ameonekana akihudhuria hafla hizo akiwa na zawadi mbalimbali, jambo ambalo limeendelea kuwavutia mashabiki wake.
Wakati huohuo, picha zinazoonyesha Jux akiwa hajavaa shati zimeendelea kusambaa, huku baadhi ya mashabiki wakizilinganisha na mwonekano wake wa sasa baada ya kufunga ndoa.
Mabadiliko hayo ya mwonekano na maisha ya Jux baada ya ndoa yamekuwa yakifuatiliwa kwa karibu na mashabiki, huku Priscilla naye akionekana kufurahia safari hiyo pamoja na mumewe.



