Afrika Mashariki

Okwi atangaza kustaafu soka la kulipwa

...aahidi kuendelea kukuza vipaji

DAR ES SALAAM: Mchezaji wa zamani wa Simba SC na nahodha wa zamani wa Timu ya Taifa ya Uganda (Uganda Cranes), Emmanuel Arnold Okwi, ametangaza rasmi kustaafu soka la kulipwa, akihitimisha safari yake ya miaka mingi katika mchezo huo.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, Okwi amesema uamuzi wa kustaafu ni miongoni mwa maamuzi magumu zaidi kuwahi kufanya maishani mwake, akieleza kuwa soka halikuwa kazi tu bali lilikuwa ndoto, shauku na kusudi la maisha yake.

Amesema kuichezea Timu ya Taifa ya Uganda na kuvaa jezi ya Uganda Cranes ni heshima kubwa aliyowahi kuipata katika maisha yake ya soka, huku akibainisha kuwa kubeba kitambaa cha unahodha ni jambo atakalolihifadhi moyoni daima.

Okwi pia ametoa shukrani kwa klabu zote alizowahi kuzitumikia, makocha, wachezaji wenzake, wapinzani pamoja na mashabiki kwa mchango wao katika mafanikio aliyoyapata ndani na nje ya uwanja.

Licha ya kutundika daruga, nyota huyo amesema hatajitenga na mchezo wa soka, akisisitiza kuwa ataendelea kushiriki katika maendeleo ya mchezo huo kwa kusaidia kukuza vipaji na kuhamasisha kizazi kijacho cha wachezaji kufikia ndoto zao.

Related Articles

Back to top button