Ligi Kuu

Yanga yaongeza nguvu benchi la Ufundi

DAR ES SALAAM: YANGA imewatambulisha wataalamu watatu kutoka Afrika Kusini, Simo Dladla, Kagisho Dikgacoi na Yardaan Valodia, watakaofanya kazi chini ya Kocha Mkuu Manqoba Mngqithi.

Dladla ametambulishwa kuwa Kocha Msaidizi akija na uzoefu wa kufanya kazi katika klabu za Richards Bay, Maritzburg United, Maroka Swallows, Golden Arrows na Mamelodi Sundowns.
Mbali na Dladla, mabingwa hao watetezi wamemtambulisha Kagisho Dikgacoi ambaye atakuwa kocha wa mbinu za mipira ya adhabu ‘Set Piece Coach’.

Dikgacoi amewahi kufanya kazi Fulham, Crystal Palace, Cardiff City pamoja na timu ya taifa ya Afrika Kusini.

Yanga pia imemtambulisha Yardaan Valodia ambaye atahudumu kama Kocha mchambuzi wa takwimu akitarajiwa kuchambua utendaji wa timu na wapinzani kwa kutumia takwimu na teknolojia ili kusaidia benchi la ufundi kufanya maamuzi ya kiufundi.

Pia, imemtambulisha kocha wa magolikipa Greg Etafia aliyewahi kufanya kazi Moroka Swallows ya Afrika Kusini na timu za taifa za vijana nchini Nigeria.

Ujio wa wataalamu hao unaongeza nguvu kwenye benchi la Mngqithi, ambaye ametua Jangwani kwa lengo la kuendelea kuifanya Yanga iwe na ushindani mkubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa msimu wa 2026/27.

Kwa maboresho hayo, ni wazi Yanga imeamua kuwekeza si tu kwa wachezaji, bali pia katika idara ya ufundi kwa lengo la kuongeza ubora wa maandalizi na ushindani wa kikosi chake.

Mwisho

Related Articles

Back to top button