Coastal yatimkia Mara, yazifuata Leopards, Shabana

DAR ES SALAAM: COASTAL Union imechagua njia tofauti ya kuanza safari ya msimu mpya. Badala ya kubaki Tanga, Wagosi wa Kaya wamehamishia kambi yao mkoani Mara, huku wakipanga kuvaana na vigogo wa Kenya, AFC Leopards na Shabana FC, katika mechi za kirafiki za kujiandaa na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ofisa Habari wa Coastal Union, Hussein Mchomvu ‘Diego’, amesema kikosi kiliripoti kambini Julai 20 na benchi la ufundi limeamua kwenda Mara ili kuwapa wachezaji mazingira mapya ya maandalizi pamoja na kupata mechi zenye ushindani.
“Tumeamua kwenda Mara kwa sababu tulihitaji mazingira tofauti yatakayowapa wachezaji uzoefu mpya. Pia tumefanikiwa kupata mechi mbili za kirafiki dhidi ya AFC Leopards na Shabana kutoka Kenya,” amesema Mchomvu.
Amesema kikosi kinatarajia kuondoka Agosti 3 kuelekea Mara, ambapo kitacheza mechi hizo Agosti 6 na 9 kabla ya kurejea Tanga kuendelea na maandalizi ya mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa FC.
Mchomvu amesema maandalizi yanaendelea vizuri na malengo yao ni kuanza msimu kwa nguvu ili kukusanya pointi nyingi mapema na kupunguza presha katika hatua za mwisho za ligi.
Kuhusu kikosi, amesema klabu hiyo imepunguza idadi ya wachezaji baada ya kuwaaga saba kati ya 34 waliokuwapo, huku 27 wakiendelea kubaki na usajili wa nyota wapya ukiwa umekamilika kwa baadhi yao.
“Baadhi ya usajili tumeshakamilisha na tunaamini msimu huu hautakuwa rahisi kwa timu yoyote kuja kuchukua pointi Mkwakwani,” amesisitiza.




