Kichapo kilivyompa Katwila hasira

LINDI: KOCHA wa Geita Gold Zuberi Katwila amesema kukasirika na kuwakemea wachezaji wake wakati wa mchezo si jambo la ajabu, akieleza kuwa hatua hiyo ilikuwa sehemu ya kusimamia maelekezo aliyowapa na kuhakikisha timu inafanya vizuri zaidi uwanjani.
Timu hiyo imetoka kupoteza mchezo uliopita kwa bao 1-0 dhidi ya Namungo Ugenini, matokeo yaliyoonekana kumpa hasira.
Kocha huyo amesema kabla ya mchezo walikuwa wameandaa namna ya kucheza, lakini mpira unapofika uwanjani huwezi kutabiri kila kitakachotokea kwa sababu wanakutana na wapinzani ambao nao wana uwezo wa kubadilisha mambo.

“Huu ni mchezo wa mpira, wanacheza na binadamu. Unaweza kuandaa, lakini ikafika uwanjani kuna vitu vikabadilika. Kwa hiyo lazima uweze kusimamia. Kama kocha, lazima niweze kukasirika kwa maana nataka kufanya vizuri zaidi na mimi niwe nimehakikisha kazi ambayo nimeiandaa inatekelezwa,” amesema.
Amesema hata pale anapowakemea wachezaji kutokana na makosa wanayofanya, lengo si kuwakatisha tamaa bali kuwafanya warekebishe makosa na kuendelea kupambana.
Akizungumzia mchezo huo, kocha amesema wapinzani wao waliweza kutumia nafasi walizozipata na kufunga bao moja, huku upande wao ukishindwa kutumia nafasi walizotengeneza.
Amesema hakuna muda wa kulalamikia matokeo kutokana na ratiba kuwa ngumu, akieleza kuwa timu ina siku mbili pekee za kujiandaa na kusafiri kwa ajili ya mchezo unaofuata.
Katwila amesema jambo la msingi ni kutulia, kuchambua makosa yaliyofanyika katika mchezo uliopita na kuyafanyia kazi ili timu iweze kufanya vizuri katika mchezo unaofuata.



