Mobetto: Siwezi kuvunja mawasiliano na Majizzo

DAR ES SALAAM: Msanii wa Bongo Fleva na mfanyabiashara, Hamisa Mobetto, amesema haoni sababu ya kusitisha mawasiliano na mzazi mwenzake, Majizzo, kwa kuwa wote wana wajibu wa kushirikiana katika malezi ya mtoto wao, Fantasy.
Akizungumza kuhusu uhusiano wao wa sasa, Hamisa amesema mawasiliano kati yake na Majizzo yanahusu ustawi wa mtoto wao na hayapaswi kuzuiwa na hali ya sasa ya maisha ya kila mmoja.
“Mimi na Majizzo lazima tuongee kwa ajili ya mtoto wetu. Ni kweli kuna kipindi tulikaa muda bila kuongea wala kusalimiana, lakini baadaye nikaona haina maana. Tunamuumiza tu mtoto.
Kwa nini tusisalimiane au Majizzo asiwe karibu na mtoto wake kwa sababu ameoa? Wangapi wameoa na bado wanaendelea kuwalea na kuwajali watoto wao?” amesema Hamisa.
Hamisa amesisitiza kuwa maslahi ya mtoto yanapaswa kuwa kipaumbele kwa wazazi wote, akieleza kuwa ushirikiano na mawasiliano mazuri kati ya wazazi huchangia ukuaji na ustawi wa mtoto.
Kauli yake imeibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya wadau wakieleza kuwa malezi bora yanahitaji wazazi kushirikiana kwa manufaa ya watoto wao bila kujali mabadiliko ya maisha binafsi.




