Filamu

Couple Goals yaitangaza Tanzania,

...yakabidhi tuzo mbili za ZIFF kwa bodi ya filamu

DAR ES SALAAM: MTAYARISHAJI wa filamu na mwigizaji, Lilian Shirima, ametembelea Bodi ya Filamu Tanzania na kuwasilisha tuzo mbili zilizotwaliwa na filamu ya Couple Goals katika Tamasha la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) 2026.

Filamu hiyo ilijinyakulia Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike Tanzania, iliyotwaliwa na Chuchu Hansy, pamoja na Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kiume Tanzania, iliyotwaliwa na Prince Jimmy, mafanikio yanayoendelea kuonesha kukua kwa tasnia ya filamu nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Asha Ngatila, amewapongeza watayarishaji, waigizaji na wadau wote walioshiriki kufanikisha filamu hiyo, akisema ushindi huo ni kielelezo cha ubora na ushindani wa filamu za Tanzania katika majukwaa ya kimataifa.

Amesema Bodi ya Filamu Tanzania itaendelea kushirikiana na wanatasnia kwa kuwapa mazingira wezeshi yatakayochochea ubunifu, weledi na uzalishaji wa kazi zenye viwango vya kimataifa.

Aidha, Ngatila alitoa wito kwa wanawake wanaojishughulisha na sekta ya filamu nchini kuendelea kujiamini, kufanya kazi kwa bidii na kutumia ipasavyo fursa zilizopo ili kufikia mafanikio makubwa zaidi katika tasnia hiyo.

Kwa upande wake, Lilian Shirima ameishukuru Bodi ya Filamu Tanzania kwa mchango wake katika maendeleo ya filamu ya Couple Goals, ameeleza kuwa ushirikiano uliotolewa kuanzia usajili wa filamu, utoaji wa vibali vya utayarishaji, usambazaji na upangaji wa daraja umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yaliyowezesha filamu hiyo kutwaa tuzo hizo muhimu katika ZIFF 2026.

Katika hafla hiyo, mshindi wa Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike Tanzania, Chuchu Hansy, aliwakilishwa na Stellabeatrice Benedict.

Bodi ya Filamu Tanzania imeeleza kuwa itaendelea kutambua, kuhamasisha na kuunga mkono mafanikio ya watayarishaji na wasanii wa filamu wanaoipeperusha vyema bendera ya Tanzania kupitia kazi zao ndani na nje ya nchi.

Related Articles

Back to top button