Kwingineko

England, Argentina nani kumfuata Hispania?

ATLANTA: England na Argentina zinashuka dimbani leo katika nusu fainali ya Kombe la Dunia zikiwa na lengo moja la kutinga fainali, huku historia ndefu ya ushindani kati ya mataifa hayo ikiongeza uzito wa pambano hilo litakalochezwa Atlanta.

Kocha wa England, Thomas Tuchel, amesema jukumu lake kubwa kabla ya mchezo huo ni kuhakikisha wachezaji wake hawabanwi na presha ya historia ya mechi hiyo, bali wanaelekeza nguvu zao kwenye mpango wa mchezo pekee.

“Kwa kocha, hili ni pambano la soka tu. Hatuzungumzii matukio ya kihistoria, tunawapa wachezaji ujumbe rahisi ili waweze kutekeleza majukumu yao uwanjani,” amesema Tuchel.

Amekiri kuwa haiwezekani kupuuza ukubwa wa mchezo huo kutokana na historia ya ushindani kati ya England na Argentina, ambayo imewahi kugubikwa na matukio makubwa ya kisoka na hata mvutano wa kisiasa.

Kwa upande wake, kocha wa Argentina, Lionel Scaloni, amesisitiza kuwa mchezo huo haupaswi kuhusishwa na Vita vya Falklands vya mwaka 1982, akieleza kuwa kilichopo sasa ni mpira wa miguu pekee.

“Huu ni mchezo wa soka. Sitaki kuchanganya mambo yaliyotokea zamani na mechi ya leo. Ni historia yenye huzuni, lakini sasa tunacheza mpira,” amesema Scaloni.

Scaloni ameongeza kuwa bao maarufu la Diego Maradona la mwaka 1986 dhidi ya England litaendelea kubaki sehemu muhimu ya historia ya soka ya Argentina.

England inaingia kwenye mchezo huo baada ya kuiondoa Norway robo fainali kwa ushindi uliopatikana baada ya muda wa nyongeza, huku Tuchel akitaka kikosi chake kipunguze makosa ya kiufundi na kuongeza ubora katika mashambulizi.

Argentina nayo imepitia safari ngumu katika hatua za mtoano, ikicheza muda wa nyongeza mara mbili na kutoka nyuma kwa mabao mawili kuiondoa Misri katika hatua ya 16 bora.

Mshindi wa pambano hilo atatinga fainali ya Kombe la Dunia na kukutana na Hispania, ambayo tayari imefuzu baada ya kuiondoa Ufaransa kwa ushindi wa mabao 2-0.

Related Articles

Back to top button