World Cup

Hispania, Ubelgiji kukiwasha leo kusaka nusu fainali Kombe la Dunia

LOS ANGELES: Mabingwa wa Ulaya, Hispania, watashuka dimbani leo kuikabili Ubelgiji katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Dunia 2026 wakisaka tiketi ya kutinga nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu walipotwaa taji hilo mwaka 2010.

Mchezo huo utakaopigwa katika Uwanja wa Los Angeles nchini Marekani unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku mshindi akikutana na Ufaransa iliyowatoa Morocco kwa ushindi wa mabao 2-0.

Hispania imekuwa moja ya timu zilizovutia kwenye michuano hiyo kutokana na safu yake imara ya ulinzi. Imeweka rekodi ya kutoruhusu bao katika mechi sita mfululizo za Kombe la Dunia, ikiwemo ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Austria na 1-0 dhidi ya Ureno uliomaliza safari ya Cristiano Ronaldo.

Katika hatua ya makundi, Hispania iliongoza Kundi H kwa pointi saba baada ya kuzifunga Saudi Arabia na Uruguay huku ikitoka sare dhidi ya Cape Verde.

Kwa upande wa Ubelgiji, timu hiyo iliongoza Kundi G kwa pointi tano baada ya kuifunga New Zealand na kutoka sare dhidi ya Iran na Misri. Katika hatua ya mtoano iliiondoa Senegal kwa ushindi wa mabao 3-2 baada ya muda wa nyongeza kabla ya kuichapa wenyeji Marekani mabao 4-1.

Kipa wa Ubelgiji, Thibaut Courtois, amesema wachezaji wanaamini wana uwezo wa kuiondoa Hispania licha ya ubora wa wapinzani wao.

“Kila mmoja kwenye timu anaamini inawezekana. Tuna kikosi chenye uwezo mkubwa na Hispania italazimika kutuheshimu. Daima kuna matokeo ya kushangaza na tunaamini tunaweza kuwa moja ya mshangao wa michuano hii,” alisema Courtois.

Ubelgiji inategemea uzoefu wa nyota wake Kevin De Bruyne na Romelu Lukaku, ambaye ndiye kinara wa mabao wa timu hiyo akiwa amefunga mabao matatu. Wengine wanaotegemewa ni Leandro Trossard, Charles De Ketelaere na Youri Tielemans.

Hispania kwa upande wake itaendelea kumtegemea mshambuliaji Mikel Oyarzabal, aliyefunga mabao manne kwenye michuano hiyo, pamoja na winga chipukizi Lamine Yamal, ambaye kiungo Dani Olmo amesema anaendelea kuimarika kadri mashindano yanavyoendelea.

Kwa mujibu wa takwimu za Opta, Hispania inapewa nafasi kubwa ya kushinda kwa asilimia 59.3 ndani ya dakika 90, huku Ubelgiji ikipewa asilimia 18.3 na uwezekano wa mchezo kwenda muda wa nyongeza ukiwa asilimia 22.4.

Related Articles

Back to top button