TPC yamteua Dk Janeth Mlay kwenye ufundi

DAR ES SALAAM: KAMATI ya Paralimpiki Tanzania (TPC) imefanya maboresho makubwa ya kiutawala na kiufundi kwa kumteua Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Janeth Mlay, kuwa Mkurugenzi wa Ufundi.
Hii ni mara ya kwanza imeanzisha kamati ya ufundi itakayosimamia maandalizi ya wanamichezo kuelekea Michezo ya Paralimpiki ya Los Angeles 2028 (LA28).
Maboresho hayo ni sehemu ya mkakati wa uongozi mpya wa TPC chini ya Katibu Mkuu, Ramadhan Namkoveka, unaolenga kutumia sayansi ya michezo kuboresha maandalizi ya wanamichezo wenye ulemavu ili kuongeza idadi ya watakaofuzu na kushindania medali katika Paralimpiki za mwaka 2028 nchini Marekani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Namkoveka amesema uteuzi wa Dk Mlay umezingatia taaluma, uzoefu na mchango wake katika maendeleo ya michezo ya watu wenye ulemavu.
Amesema Dk Mlay, ambaye pia sasa ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TPC, ana Shahada ya Uzamivu (PhD) aliyohitimu mwaka 2023 kutoka UDSM, Shahada ya Uzamili ya Falsafa katika Elimu Maalum kutoka Chuo Kikuu cha Oslo nchini Norway, pamoja na sifa nyingine za kitaaluma katika michezo na saikolojia.
“Katika awamu hii mpya, azma yetu ni kuleta mapinduzi ya kweli na kuongeza idadi ya washiriki wetu katika mashindano ya kimataifa. Tunataka Tanzania ipeleke kikosi kikubwa cha wanamichezo waliofuzu kwa viwango vya juu vya ushindani, ndiyo maana tunahitaji wataalamu waliobobea kama Dk Mlay kuongoza idara ya ufundi,” amesema.
Sambamba na uteuzi huo, TPC imetangaza wajumbe wa Kamati mpya ya Ufundi itakayoongozwa na Dk Mlay ambao ni Ida Jaribu, Innocent Jonas (Para-Swimming), Bahati Mgunda (Para-Athletics), Nemes Chiwalala (Powerlifting) na Abubakar Maganda, huku nafasi moja ikitarajiwa kujazwa ili kukamilisha kamati hiyo.
Kwa mujibu wa TPC, kamati hiyo itakuwa na jukumu la kuandaa Mpango Mkakati wa Haraka kuelekea LA28, kusimamia kalenda ya shughuli za mwaka, kuandaa kambi za maandalizi ya wanamichezo 10 hadi 15 wanaolenga kufikia viwango vya kimataifa vya kufuzu (MQS), pamoja na kuanzisha kanzidata ya kidijitali ya uainishaji wa wanamichezo nchini.
Namkoveka amevitaka vyama vya michezo vya watu wenye ulemavu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar kuendelea kujiandaa kwa kuwa dirisha la kufuzu na kupata uainishaji wa Paralimpiki za Los Angeles 2028 lilifunguliwa Januari 1, 2026 na litafungwa Julai 2, 2028.




