Serikali kutumia bilioni 15 kuondoa changamoto za matamasha Zanzibar

ZANZIBAR:SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema itatumia sh. bilioni 15 kujenga Kijiji cha Utamaduni kitakachoweka pamoja matamasha mbalimbali yanayofanyika visiwani humo, hatua inayolenga kumaliza changamoto ya ukosefu wa eneo la kudumu kwa ajili ya shughuli za sanaa na utamaduni.
Akizungumza katika hafla ya kufunga Tamasha la 29 la Kimataifa la Filamu la Nchi za Jahazi (ZIFF), Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Riziki Pembe, alisema changamoto zilizojitokeza katika maandalizi na uendeshaji wa tamasha la mwaka huu zimetokana na ukarabati unaoendelea katika eneo la Ngome Kongwe, ambalo kwa miaka mingi limekuwa kitovu cha tamasha hilo.
Alisema serikali imeidhinisha fedha hizo kwa ajili ya kujenga Kijiji cha Utamaduni chenye miundombinu ya kisasa, ikiwemo kumbi mbalimbali za maonesho na shughuli za sanaa, ili kutoa mazingira bora kwa waandaaji wa matamasha na wadau wa sekta ya ubunifu.
Dk. Pembe aliwataka wadau wa sanaa kushirikiana na serikali kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa mafanikio, akieleza kuwa ni sehemu ya maono ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ya kuimarisha sekta ya utamaduni na kuongeza mchango wake katika uchumi wa ZanziZanzibarl
Aidha, aliwataka waandaaji wa ZIFF kuhakikisha kunakuwa na ufuatiliaji wa washindi wa tuzo na wadau wengine baada ya tamasha kumalizika ili kupima namna wanavyotumia fursa walizozipata, badala ya kuishia kwenye hafla ya utoaji wa tuzo pekee.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na waandaaji wa ZIFF kwa kuwa tamasha hilo limeendelea kufungua fursa kwa vijana, kukuza tasnia ya filamu na kuitangaza Zanzibar kimataifa kupitia sanaa na utamaduni.
Naye Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Christine Grau, alisema ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na ZIFF utaendelea hata baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini. Alisema anaamini tamasha hilo lina nafasi kubwa ya kukuza simulizi za Afrika na kutumia Teknolojia ya Akili Bandia (AI) katika kuhifadhi na kuendeleza urithi wa utamaduni kupitia filamu.




