Inkaar
PICHA linaanza baada ya tukio la utekaji nyara wa mtoto wa tajiri Haridaas Chaudhary katika jengo la tajiri huyo wa kiwanda cha viatu.
Tukio hili linafanywa na Raj Singh akishirikiana na washirika wake Manmohan na Preeti.
Raj Singh anafanya tukio hilo la utekaji nyara akikusudia kulipa kisasi kwa tukio la zamani lililofanywa na Haridaas Chaudhary. Mbali na sababu hiyo, pia Raj Singh anataka alipwe fidia ya jumla ya Rupia milioni 20 kama fidia ya kumwachia mtoto huyu aliyetekwa.
Hata hivyo, Raj Singh na watekaji wenzake wanapotea maboya, badala ya kumteka nyara mtoto wa tajiri Haridaas Chaudhary wanajikuta wakifanya kosa kubwa kwa kumteka mtoto wa mtumishi wa nyumbani (Saadhu Meher).
Awali, baada ya kupata taarifa za utekaji nyara, tajiri Haridaas Chaudhary alikuwa tayari kulipa kiasi kikubwa cha fedha kama fidia kwa ajili ya mtoto wake lakini baadaye anagoma kulipa fedha hizo baada ya kugundua kuwa mtoto aliyetekwa si wake bali ni mtoto wa mtumishi wake.
Hata hivyo, baadaye anakubali kulipa fidia hiyo ili kuachiwa kwa mtoto huyo na baada ya mambo kukamilika mtoto anaachiwa, lakini askari mpelelezi Amar (Vinod Khanna) hayuko tayari kuachana na kesi hii ya utekaji nyara katika hatua hii.
Anaamua kula sahani moja na watekaji kwa kuchunguza kila hatua kwa undani juu ya kesi hii na anafuatilia nyendo zote za mtekaji mkuu, yaani, Raj Singh.
Pamoja na hayo, hakuna maelewano mazuri kati ya mpelelezi huyu na Haridaas Chaudhary kwa sababu mpelelezi Amar anatokea kumpenda sana dada wa Haridaas aitwaye Geeta (Vidya Sinha) na yupo tayari kumuoa lakini Haridaas anakataa kubariki ndoa yao.
Hata hivyo, mpelelezi Amar hataki kuruhusu hisia zake binafsi (za mapenzi) kuathiri wajibu wake wa kazi ya kuchunguza kuhusu uhalifu uliotokea.
Si tu kwamba anamkamata mtekaji Raj Singh mwishoni bali pia anafanikiwa kurudisha fedha iliyotumika kama fidia ya kumrejesha mtoto aliyetekwa…
Ni dhahiri kuwa filamu ya Inkaar inawakilisha mchezo wa paka na panya kati ya mhalifu na mpelelezi. Hii ni filamu iliyotolewa mwaka 1977, ni moja ya filamu za kusisimua sana.
Upekee wa filamu hii ya kihalifu ni kwamba inalenga kidogo juu ya uhalifu na zaidi imejikita kwenye uchunguzi wa uhalifu huo. Kwa kweli, eneo kubwa la simulizi hii limejikita katika upelelezi uliofanywa na Amar na msaidizi wake, Yadav (M. Rajan).
Script ya filamu hii imeandikwa kimantiki na kitaalamu kwa shughuli za kipelelezi na shujaa katika simulizi hii anatatua suala hilo na kumkamata mhalifu kama mtu wa kawaida tu na si kama mtu wa ajabu wa kufikirika kama ilivyo kwenye filamu nyingi za Bollywood.
Filamu hii licha ya matukio kadhaa ya kimapenzi yanayooneshwa kwenye matukio ya nyuma (flash back), inamweka mtazamaji kwenye kiti akifuatilia mtiririko wake kwa karibu saa mbili.
Mwandishi wa simulizi hii, Jyoti Swaroop na mwongozaji wa filamu, Raj N. Sippy wameweza kuifanya filamu ioneshe uhalisia na kumfanya mtazamaji ajikute kana kwamba anaangalia mambo ya kweli, na ni njia hii tu ambayo imeifanya filamu hii kuwa tofauti sana na filamu nyingi zinazotengenezwa nchini India.
Mbali na uhalifu na uchunguzi wake, filamu hii inaonesha hali ya kibinadamu pia kwa uhalisi na ukatili. Mfanyabiashara tajiri amefika kwenye nafasi yake ya sasa kutokea mazingira ya kawaida sana lakini anakataa kumuoza dada yake kwa askari mpelelezi kwa sababu tu ya utofauti wa hali ya kimaisha.
Kitaalamu filamu hii inapewa alama za juu. Tukio la kumfukuzia adui kwa mbwa wa polisi katika kilele cha simulizi ni jambo linalosisimua zaidi na kuvutia.
Filamu hii si aina ya filamu ndefu sana za Bollywood zenye masimulizi yanayochosha. Hii ni filamu yenye urefu wa dakika 132.
Hata muziki wa Rajesh Roshan uliotumika ndani ya filamu hii na utunzi wa Majrooh Sultanpuri ni wa heshima. Wimbo wa Mungda Mungda Main Gud Ki Dali ulioimbwa na Usha Mangeshkar umeendelea kuwa maarufu hata leo.
Ikumbukwe kuwa miaka ya sabini ilishuhudiwa kuibuka filamu nyingi za kihalifu katika Bollywood ingawa stori nyingi za uhalifu wakati huo zilikuwa za kawaida sana.
Ni filamu chache tu miongoni mwa filamu za kihalifu zinazotengenezwa Bollywood zilitengenezwa vizuri na zilipendwa.
Asilimia hiyo ndogo tu ya filamu za kihalifu zinazotengenezwa Bollywood zinastahili kama bidhaa bora. Kwa maana hiyo wale wanaopenda simulizi za uhalifu na upelelezi hawatakiwi kuikosa filamu hii.
Tukutane Jumamosi ijayo kwa simulizi nyingine ya filamu ya kusisimua.
0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com