Kliniki ya raga kwa wanawake kuanza kesho

DAR ES SALAAM: CHAMA cha Raga Tanzania (TRU), kupitia Idara ya Raga ya Wanawake, kinatarajia kuanza kliniki ya Raga ya Wanawake ya siku mbili yenye lengo la kukuza uwezo wa wachezaji na makocha wa raga nchini Tanzania.
Kliniki hiyo itaendeshwa na Philadelphia Orlando, nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya wanawake ya Kenya (Kenya Lionesses) na kwa sasa Kocha Mkuu wa Mpango wa Raga ya Wanawake wa Falme za Kiarabu (UAE Rugby).
Tukio hili litawakutanisha wachezaji wa raga wa wanawake kutoka klabu mbalimbali nchini kwa mafunzo maalum yatakayojikita katika mbinu za mchezo, uelewa wa raga, uongozi na maendeleo ya mwanamichezo.
Kliniki hiyo itafanyika tarehe 26 na 27 Juni 2026 katika Uwanja wa Beach Soccer, Coco Beach, Dar es Salaam, kuanzia saa 10 jioni kila siku.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho, mpango huo ni sehemu ya dhamira ya Chama cha Raga Tanzania ya kuendeleza mchezo wa raga kwa wanawake na kutoa fursa kwa wanamichezo kujifunza kutoka kwa wataalamu wa kimataifa wenye uzoefu mkubwa katika mchezo huo.
“TRU inapenda kutoa shukrani za dhati kwa UAE Rugby kwa kuunga mkono maendeleo ya raga ya wanawake nchini Tanzania, pamoja na Africraft kwa kudhamini tukio hili na kuchangia ukuaji wa michezo na ushirikishwaji wa jamii,”amesema.
Chama cha Raga Tanzania kimewahimiza wachezaji wote wa raga wa wanawake, makocha na wadau wa mchezo huo kushiriki katika fursa hii adhimu ya kujifunza kutoka kwa mmoja wa viongozi mashuhuri wa raga barani Afrika.




