Uchunguzi Kifo cha muigizaji India waendelea

MUMBAI, INDIA : Tasnia ya filamu na televisheni nchini India imegubikwa na majonzi kufuatia kifo cha ghafla cha mwigizaji chipukizi Sanchita Ugale, aliyefahamika zaidi kupitia tamthilia maarufu ya ‘Kumkum Bhagya’.
Kifo chake kimetikisa mashabiki, waigizaji wenzake na wadau wa burudani nchini humo ambapo inadaiwa Sanchita alifariki dunia katika makazi yake yaliyopo Nalasopara, jimbo la Maharashtra huku uchunguzi wa kifo chake ukiendelea licha ya taarifa zisizo rasmi kudai kwamba mwigizaji huyo alikuwa na msongo wa Mawazo kwa muda mrefu.
Marehemu alikuwa mmoja wa waigizaji waliokuwa wakijijengea jina kwa kasi katika tasnia ya televisheni, akionekana katika vipindi mbalimbali maarufu ikiwemo ‘Kumkum Bhagya’, ‘Wagle Ki Duniya’ na ‘Dilwali Dulha Le Jayegi’.
Baada ya taarifa za kifo chake kusambaa, mashabiki wengi walijitokeza kupitia mitandao ya kijamii kueleza masikitiko yao na kutoa salamu za rambirambi. Wengi walieleza kushangazwa na tukio hilo wakisema Sanchita alikuwa bado na safari ndefu ya mafanikio katika sanaa.
Wakati huo huo, familia ya marehemu imeeleza masikitiko makubwa kufuatia tukio hilo huku baba yake akidai kuwa binti yake alikuwa akipitia msongo wa mawazo na changamoto mbalimbali kabla ya kifo chake. Hata hivyo, mamlaka husika zimeeleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini ukweli wa kilichotokea.
Kifo cha Sanchita kimeibua mjadala mpana kuhusu afya ya akili miongoni mwa wasanii na vijana kwa ujumla, huku wadau mbalimbali wakisisitiza umuhimu wa kutoa msaada wa kisaikolojia kwa watu wanaokabiliwa na changamoto za maisha.




