Rosemary, Nyamhanga watamba baada ya kutwaa tuzo

DAR ES SALAAM:WASHINDI wa tuzo za wachezaji bora wa mwezi Mei katika mashindano ya mpira wa wavu nchini, Rosemary Lazier wa Bandari na Fabian Nyamhanga wa TPDC, wamesema kutwaa tuzo hizo kumewaongezea hamasa ya kufanya vizuri zaidi na kuendelea kupambania mafanikio makubwa katika timu zao.
Rosemary amesema amepokea tuzo hiyo kwa furaha kubwa kwani ilikuwa miongoni mwa malengo aliyokuwa amejiwekea msimu huu.
Amesema kutambuliwa kwa mchango wake kutamfanya kuongeza juhudi ili kuendelea kufanya vizuri katika Ligi ya DAREVA na TVNL, huku akilenga kusaidia Bandari kupata matokeo mazuri.
“Tuzo hii ni hamasa kubwa kwangu binafsi. Ni moja ya vitu nilivyokuwa navihitaji na itanifanya nijitume zaidi ili niendelee kufanya vizuri na kupata tuzo nyingine,” amesema Rosemary.

Kwa upande wake, Nyamhanga amesema mafanikio hayo yametokana na kujituma mazoezini, nidhamu na ari ya kupambana kila siku.
Mchezaji huyo wa TPDC amesema tuzo hiyo imeongeza morali kwake pamoja na wachezaji wenzake huku akisisitiza kuwa lengo lao kubwa ni kutwaa ubingwa wa Serie B msimu huu.
“Malengo yetu ni kutwaa ubingwa, huku binafsi nikitamani kushinda tuzo zote za Serie B. Nitaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo hayo,” amesema Nyamhanga.
Washindi hao walikabidhiwa tuzo hizo Dar es Salaam jana.


