
ATLANTA:USIKU wa kihistoria wa golikipa Vozinha dhidi ya Hispania haukuishia kwenye ‘saves’ zake pekee, bali pia ulimshuhudia akiondoka na tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi baada ya kuiongoza Cape Verde kupata sare ya bila kufungana.

Vozinha alikuwa shujaa mkubwa wa Cape Verde katika mchezo huo wa Kombe la Dunia 2026, akifanya saves kadhaa muhimu zilizowazuia washambuliaji wa Hispania kupata bao.
Katika dakika zote 90 za mchezo, kipa huyo mwenye umri wa miaka 40 alionesha utulivu mkubwa na uzoefu wake langoni, huku akiokoa mipira mingi ya hatari iliyokuwa ikielekea wavuni.

Kwa mujibu wa takwimu za mchezo, Vozinha alifanya saves saba ndani ya eneo la hatari, ambapo kati ya hizo, saves tatu zilikuwa ni za kuruka na nyingine 3 za kudaka mipira ya juu iliyokuwa na hatari kwa lango lake.
Kiwango hicho ndicho kilichompa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi na kumfanya kuwa gumzo kubwa miongoni mwa mashabiki wa soka duniani.
Mbali na tuzo hiyo, Vozinha pia ameandika historia ya Kombe la Dunia kwa kuwa kipa mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kutunza ‘clean sheet’ katika mechi yake ya kwanza kwenye mashindano hayo, akiwa na miaka 40.

Kwa Cape Verde, matokeo hayo ni moja ya kurasa muhimu zaidi katika historia ya soka la taifa hilo. Na kwa Vozinha binafsi, ulikuwa usiku ambao utaendelea kukumbukwa kwa miaka mingi ijayo.
Vozinha ameonesha kuwa umri ni namba tu pale unapokuwa na ubora, uzoefu na moyo wa kupambana.




