Maajabu ya Kombe la Dunia 2026 haya hapa

MACHO ya dunia leo yanaelekezwa kwenye kuanza rasmi kwa Kombe la Dunia 2026 ambalo linaingia kwenye historia kama toleo kubwa zaidi kuwahi kuandaliwa tangu mashindano hayo yaanze.
Kwa mara ya kwanza, mashindano hayo yanafanyika kwa mfumo mpya wenye timu 48 badala ya timu 32 zilizokuwa zikishiriki miaka iliyopita.
Mbali na ongezeko la timu, Kombe la Dunia la mwaka huu litakuwa na jumla ya michezo 104, idadi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya mashindano hayo.

Mfumo huo mpya unatarajiwa kutoa nafasi kwa mataifa mengi zaidi kuonesha uwezo wao kwenye mashindano hayo yanayoanza leo usiku.
Jambo jingine linalotikisa dunia ya soka ni kwamba kwa mara ya kwanza kabisa, Kombe la Dunia linaandaliwa na nchi tatu kwa pamoja ambazo ni Marekani, Mexico na Canada huku mashindano hayo yakitarajiwa kufanyika katika miji 16 tofauti.
Katika hatua nyingine ya kipekee, FIFA imeandaa sherehe tatu tofauti za ufunguzi badala ya sherehe moja ya kawaida. Kila nchi mwenyeji itakuwa na nafasi ya kuonesha utamaduni wake, burudani na historia yake mbele ya mamilioni ya mashabiki duniani. Sherehe ya kwanza inaanza leo nchini Mexico ikiwa na maonesho makubwa ya muziki, ngoma na burudani kabla ya mchezo wa ufunguzi.
Mchezo wa kwanza wa mashindano haya unawakutanisha wenyeji Mexico dhidi ya Afrika Kusini kwenye uwanja maarufu wa Mexico City Stadium (Azteca), uwanja unaoingia tena kwenye historia kwa kuwa wa kwanza duniani kuwa mwenyeji wa mechi za ufunguzi wa Kombe la Dunia mara tatu.

Mashabiki pia wanazungumzia kwa hamasa ujio wa mataifa mapya kwenye mashindano haya, yakiwemo Jordan, Uzbekistan, Cabo Verde na Curaçao ambayo yamevutia hisia za wengi wakati waliposhindania kufuzu.
Kwa upande wa teknolojia na burudani, FIFA imeongeza ladha mpya kwa kuzindua mchezo wa kidijitali unaohusiana na Kombe la Dunia kwa kushirikiana na Netflix Games ili kuwapa mashabiki nafasi zaidi na mashindano hayo.
Kadri pazia la Kombe la Dunia linavyofunguliwa leo, macho ya Afrika pia yanaelekezwa kuona kama mfumo huu mpya wa timu 48 utafungua ukurasa mpya wa mafanikio kwa mataifa ya bara hilo katika mashindano hayo makubwa zaidi ya soka duniani.




