Watatu Arsenal watajwa kuwania tuzo mchezaji bora

LONDON: WACHEZAJI watatu wa mabingwa wa Ligi Kuu England, Arsenal wameingia kwenye orodha ya wanaowania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka ya Chama cha Wachezaji wa Kulipwa England (PFA).
Walioteuliwa kutoka Arsenal ni kiungo Declan Rice, beki Gabriel Magalhaes na kipa David Raya, ambao walikuwa sehemu muhimu ya kikosi kilichoiongoza Arsenal kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 22.
Wachezaji hao watachuana Pamoja na Bruno Fernandes wa Manchester United na nyota wa Manchester City Erling Haaland na Rayan Cherki.
Fernandes anaingia kwenye kinyang’anyiro hicho akiwa na rekodi ya pasi 21 za mabao katika msimu wa Ligi Kuu England, huku akisaidia Manchester United kumaliza nafasi ya tatu. Hivi karibuni pia alitwaa tuzo ya Mwandishi Bora wa Mpira wa Miguu (FWA), ambayo mara nyingi huonekana kuwa kiashiria cha mshindi wa tuzo ya PFA.
Kwa upande wake, Haaland alimaliza msimu akiwa mfungaji bora wa ligi kwa mabao 27, wakati Cherki aling’ara katika msimu wake wa kwanza England kwa kuonesha kiwango bora kilichomfanya pia kuingia kwenye orodha ya wanaowania Tuzo ya Mchezaji Kijana Bora wa Mwaka.
Katika kipengele hicho cha vijana, Cherki ataungana na mwenzake huyo wa Manchester City, pamoja na kiungo wa Manchester United .
Majina mengine yaliyotajwa ni mshambuliaji wa Bournemouth Eli Junior ambaye alifunga mabao 13 katika mechi 33 za kwanza za Ligi Kuu England, pamoja na vijana wa Arsenal Max Dowman na Rio Ngumoha.
Washindi wa tuzo hizo wanatarajiwa kutangazwa Agosti 25 katika hafla ya 53 ya Tuzo za PFA itakayofanyika jijini Manchester.




