Muziki

Bingwa wa R&B na mshindi wa Grammy Peabo Bryson afariki dunia

NEW YORK: ULIMWENGI wa muziki wa R&B umeingia kwenye majonzi baada ya kupokea taarifa za kifo cha gwiji wa muziki huo Peabo Bryson, ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 75.

Bryson aliyewahi kushinda tuzo za Grammy akiwa sambamba na Celine Dion kupitia wimbo wa ‘Beauty and the Beast’, atakumbukwa na nyimbo zake mbalimbali ukiwemo ‘Feel the Fire’, ‘I’m So Into You’, ‘Can You Stop the Rain’, ‘If Ever You’re in My Arms Again’ pamoja na ‘Reaching for the Sky’.

Kwa mujibu wa familia yake, mwanamuziki huyo alifariki Jana jioni akiwa amezungukwa na ndugu pamoja na watu wake wa karibu. Ingawa chanzo rasmi cha kifo hakijawekwa wazi, taarifa mbalimbali zinaeleza kuwa Bryson alipata kiharusi mwishoni mwa wiki iliyopita kabla ya kulazwa kwa matibabu.

Peabo Bryson ameondoka akiwa ameacha historia kubwa katika muziki wa R&B baada ya kutamba kwa zaidi ya miongo mitano akiwa jukwaani. Mashabiki wengi watamkumbuka kupitia vibao vyake maarufu.

Hata hivyo, jina lake litabaki kwenye mioyo ya mamilioni ya watu duniani kupitia nyimbo za Disney zilizotikisa vizazi mbalimbali. Mwaka 1992 alishinda tuzo ya Grammy akiwa sambamba na Celine Dion kupitia wimbo wa ‘Beauty and the Beast’, kabla ya kurejea tena mwaka uliofuata na kutwaa Grammy nyingine akiwa na Regina Belle kupitia ‘A Whole New World’ kutoka filamu ya ‘Aladdin’.

Familia yake imesema sauti yake ilikuwa sehemu ya kumbukumbu za furaha, mapenzi na matumaini kwa watu wengi duniani.

Ingawa ameondoka, nyimbo zake zitaendelea kuishi na kubeba kumbukumbu za sauti bora zaidi kuwahi kutokea katika muziki wa R&B.

Related Articles

Back to top button