Nyumbani

Twiga Stars, Malawi kutafuta nguvu ya WAFCON

DAR ES SALAAM: TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, leo itashuka dimbani kuikabili timu ya taifa ya wanawake ya Malawi katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki utakaochezwa Uwanja wa KMC Complex kuanzia saa 10:00 jioni.

Kocha Msaidizi wa Twiga Stars, Edna Lema, amesema mchezo huo una umuhimu mkubwa kwa timu zote mbili kwani ni sehemu ya maandalizi kuelekea fainali za Mataifa ya Afrika (Wafcon).

Edna amesema ushindi katika mchezo huo utasaidia kuongeza morali na kuijenga timu kisaikolojia pamoja na kiushindani kabla ya mashindano hayo makubwa ya bara Afrika.

“Malawi na Tanzania zote zinaelekea WAFCON, hivyo mechi hii itatupa picha halisi ya kiwango cha maandalizi yetu na maeneo ambayo bado yanahitaji maboresho kabla ya mashindano kuanza,” amesema.

Ameeleza kuwa benchi la ufundi litatumia mchezo huo kupima uwezo wa wachezaji mmoja mmoja na kikosi kwa ujumla, pamoja na kutathmini utayari wa timu kuelekea majukumu ya kimataifa yaliyo mbele yao.

Kwa upande wake, kocha wa timu ya taifa ya wanawake ya Malawi, Lovemore Fazili, amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo huo na kinautazama kama sehemu muhimu ya maandalizi ya WAFCON.
Fazili amesema wanatarajia kupata ushindani mkubwa kutoka kwa Twiga Stars, huku mechi hiyo ikiwapa fursa ya kupima uwezo wa kikosi chake na kubaini maeneo yanayohitaji kuimarishwa kabla ya kuanza kwa mashindano hayo yajayo.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa kipimo muhimu kwa timu zote mbili katika maandalizi yao ya mashindano ya Afrika, huku makocha wakitarajia kuona maendeleo ya vikosi vyao katika masuala ya mbinu, utimamu na ushindani wa kimataifa.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button