Edna: Nipo benchi la ufundi kujifunza, sio kushindana na mtu yeyote

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga Princess, Edna Lema, amesema kuwa uwepo wake kwenye benchi la ufundi la timu ya wakubwa ya Yanga ni kwa ajili ya kujifunza zaidi kuhusu kazi ya ukocha kwenye ngazi ya juu, na sio kushindana na mtu yeyote.
Akizungumza baada ya mchezo kati ya Yanga na Coastal Union, Edna alisema kuwa hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza kuwa sehemu ya benchi la ufundi la timu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, na anaichukulia kama fursa ya kipekee ya kujifunza mambo mapya ya kiufundi.
“Nimekuja kujifunza. Mechi ya Coastal Union ilikuwa ya kwanza kwangu kuwa kwenye benchi la timu ya wakubwa. Ulikuwa ushindi muhimu kwa Yanga, hasa ukizingatia mechi zinavyokuja kwa kasi. Ni muhimu kujua namna ya kupambana unapocheza nyumbani na nini cha kufanya ili kupata ushindi,” alisema Edna.
Kocha huyo wa Yanga Princess aliongeza kuwa ameweza kuona namna ambavyo presha ya mechi za nyumbani inavyowakumba makocha na wachezaji, na hilo litamsaidia kuboresha mbinu zake katika timu yake.
“Ninaendelea kujifunza. Sitaishia kwenye huu mchezo pekee. Nitahudhuria mazoezi zaidi ili kuendelea kupata ujuzi,” aliongeza Edna.
Kwa sasa, Edna anasema anathamini kila nafasi anayopata kuwa karibu na benchi la ufundi la timu ya wakubwa, akiamini kuwa uzoefu huo utamsaidia kuwa kocha bora zaidi kwa timu yake ya Yanga Princess.