Serikali yarekebisha tatizo la kutohama kwa maji kwa Mkapa

DAR ES SALAAM: SERIKALI kupitia Msemaji wake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, imesema imeleta wataalamu kutoka Uturuki kwa ajili ya kurekebisha changamoto ya kutohama kwa maji katika eneo la kuchezea (pitch) la Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Msigwa amesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya changamoto iliyojitokeza katika mchezo wa kimataifa kati ya klabu ya Simba na Al Masry, ambapo maji yalishindwa kuhama kutoka eneo la kuchezea, hali iliyozua maswali kutoka kwa wadau wa soka.
“Serikali imeleta wataalamu maalum wa uwanja wa mpira wa miguu kutoka Uturuki ambao kwa sasa wako Dar es Salaam na wanashughulikia maboresho ya uwanja huo pamoja na viwanja vitano vya mazoezi vitakavyotumika katika michuano ya AFCON,” alisema Msigwa.
Ameeleza kuwa kazi ya marekebisho ya dharura tayari imeanza, na wataalamu hao wametabiri kuwa kazi hiyo itakamilika ndani ya wiki mbili hadi tatu.
Msigwa amefafanua kuwa ukarabati mkubwa hauhusishi moja kwa moja eneo la kuchezea, bali sehemu nyingine za jengo la uwanja na mifumo ya usafirishaji wa maji.
“Pitch ya sasa ilitengenezwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wakati wa mashindano ya African Football League (AFL), walituhakikishia kuwa inaweza kutumika kwa miaka miwili kabla ya kuondolewa tabaka la juu na kupandwa nyasi mpya,” aliongeza.
Amesisitiza kuwa changamoto ya sasa ni ya muda mfupi, na baada ya ukarabati huo, uwanja utakuwa tayari kutumika kwa mashindano ya CHAN. Baada ya CHAN, serikali inapanga kuondoa kabisa tabaka la juu la uwanja na kupanda nyasi mpya kwa ajili ya matumizi ya muda mrefu.
Katika hatua nyingine, Msigwa amesema maboresho ya awali ya uwanja huo yamehusisha pia mifumo ya maji, umeme, pamoja na uwekaji wa viti vipya. Kufikia sasa, viti 16,000 vimeanza kufungwa kati ya 40,000 vilivyowasili nchini, matarajio ni kukamilisha maboresho yote ya uwanja huo ifikapo Juni 15, 2025.
Mbali na uwanja huo, serikali inaendelea na mpango wa ujenzi wa kituo kipya cha matukio ya michezo na sanaa (Sports and Arts Arena ) katika eneo la Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam. Lengo ni kuupumzisha uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya shughuli nyingi zisizo za michezo.