Tennis

Serena Williams arejea kwenye Tenisi baada ya miaka minne

MALKIA wa tenisi duniani, Serena Williams, amethibitisha rasmi kurejea kwenye mchezo huo baada ya kukaa nje kwa karibu miaka minne, jambo lililowafurahisha mashabiki wake duniani kote.

Serena, ambaye hakuwahi kucheza mechi rasmi tangu mwaka 2022, alitangaza kurejea kwake kupitia video ya matangazo ya Nike iliyokuwa na ujumbe wa “Guess everybody heard the news.”

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 44 amesema kuwa mashindano ya Queen’s Club jijini London ndiyo sehemu sahihi ya kuanza ukurasa mpya wa maisha yake ya tenisi.

“Queen’s Club inaonekana kuwa sehemu kamili ya kuanza hatua hii mpya. Uwanja wa nyasi umenipa kumbukumbu nyingi za kipekee katika maisha yangu ya tenisi na ninafurahia kurejea tena,” alisema Serena.

Ataanza safari yake mpya katika mashindano ya wawili wawili (doubles) baada ya kupewa nafasi maalum ya kushiriki. Serena atacheza sambamba na chipukizi wa Canada, Victoria Mboko.

Kwa muda mrefu kulikuwa na uvumi kuhusu kurejea kwake, hasa baada ya kuonekana akifanya mazoezi makali nchini Marekani na kurejea kwenye mfumo wa vipimo vya dawa za kusisimua misuli.

Serena anashikilia rekodi ya mataji 23 ya Grand Slam katika enzi ya mashindano ya Open Era na anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi kuwahi kucheza tenisi.

Mashabiki sasa wanasubiri kuona kama kurejea kwake kutamfikisha pia katika mashindano ya Wimbledon, ambayo amewahi kuyatwaa mara saba.

Related Articles

Back to top button