Simba hawana utani, wameingia kambini

DAR ES SALAAM: KIKOSI cha Simba SC leo Jumatatu kimerejea mazoezini kuanza maandalizi ya michezo saba iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB kabla ya kuhitimishwa kwa msimu huu.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema wachezaji wote ambao hawapo kwenye majukumu ya timu za taifa wameripoti kambini na kuanza programu ya mazoezi baada ya kumalizika kwa mapumziko ya siku saba.
Ahmed amesema kikosi hicho kimeingia katika hatua muhimu ya maandalizi huku kikilenga kumaliza msimu kwa matokeo mazuri katika mashindano yote mawili kinayoshiriki.
“Leo Jumatatu kikosi kimerejea mazoezini kujiandaa na michezo yetu saba ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho iliyobaki ya kuhitimisha msimu. Wachezaji wote ambao hawapo kwenye majukumu ya timu za taifa wapo mazoezini. Ilikuwa ni likizo ya siku saba na wote wamesharejea tayari kwa kuanza programu ya mazoezi,” amesema Ahmed.
Kabla ya kwenda kwenye mapumziko hayo, Simba ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate katika mchezo wake wa mwisho wa mashindano ya ligi.
Wekundu wa Msimbazi sasa wanajiandaa na mchezo wao ujao dhidi ya Pamba Jiji FC utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam, wakilenga kuendeleza mwenendo wao mzuri wa ushindi.




