Ancelotti afunguka kuhusu nafasi ya Neymar Kombe la Dunia

BRASILIA: KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Carlo Ancelotti amesema uamuzi wa kumjumuisha nyota Neymar Junior kwenye kikosi cha Kombe la Dunia 2026 utategemea uwezo wake wa kimwili na kiwango chake uwanjani, si hisia au umaarufu wake.
Ancelotti amesema Neymar bado ni mchezaji muhimu kwa Brazil kutokana na kipaji chake kikubwa, lakini ameathiriwa na majeraha ya muda mrefu yaliyomfanya kushindwa kuwa kwenye kiwango bora kwa kipindi kirefu.
“Neymar ni mchezaji muhimu kwa taifa hili kutokana na kipaji chake, lakini amepitia changamoto za majeraha. Kwa sasa anaendelea vizuri na ameanza kucheza mara kwa mara, hivyo tunapaswa kupima faida na hasara kabla ya kufanya uamuzi,” amesema Ancelotti katika mahojiano maalumu na Reuters.

Kocha huyo raia wa Italia amesema anaelewa Neymar anapendwa na mashabiki pamoja na wachezaji wenzake, lakini hilo halitabadilisha maamuzi yake ya kitaalamu kuhusu kikosi cha Brazil kitakachokwenda kwenye michuano hiyo.
“Ninajua Neymar anapendwa sana na wachezaji pamoja na mashabiki. Lakini mwisho wa siku, mimi ndiye mwenye jukumu la kufanya uamuzi sahihi kwa ajili ya timu,” amesema.
Ancelotti pia amesema hana presha kutoka kwa mtu yeyote kuhusu kumuita Neymar, akisisitiza kuwa atazingatia tu kiwango chake cha soka na uwezo wake wa kucheza kwa kasi inayohitajika kwenye mfumo wa timu hiyo.
Kwa mujibu wa Ancelotti, Neymar ameonesha dalili za kurejea kwenye kiwango chake katika michezo ya hivi karibuni akiwa na Santos FC baada ya kuboresha utimamu wake wa mwili.
Neymar ambaye ni mfungaji bora wa muda wote wa Brazil bado anapambana kurejea katika ubora wake kuelekea Kombe la Dunia 2026 litakaloanza mwezi ujao.




