Nyumbani

Tuzo za wanamichezo bora kutolewa kesho

DAR ES SALAAM: MSIMU wa nne wa Tuzo za Wanamichezo bora Tanzania unatarajiwa kufanyika kesho, huku waandaaji wakieleza kuwa maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya hafla hiyo ya kuwaenzi wanamichezo waliofanya vizuri ndani na nje ya nchi mwaka 2025.

Akizungumza kuelekea hafla hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha amesema tuzo hizo zitawatambua wanamichezo walioonesha kiwango bora kuanzia Januari hadi Desemba mwaka uliopita.

Msitha amesema mwaka huu kutakuwa na vipengele 21 vya tuzo vinavyogusa kada mbalimbali za michezo, tofauti na mwaka 2024 ambapo kulikuwa na vipengele 20 pekee.

Ameeleza kuwa ongezeko hilo limetokana na kuanzishwa kwa kipengele kipya cha Tuzo ya Mwanahabari Nguli wa Michezo, kitakachotambua mchango wa wanahabari waliotoa huduma kubwa katika maendeleo ya michezo nchini.

Baadhi ya vipengele vitakavyotolewa ni pamoja na Mwanamichezo Bora wa Kike na Kiume, Chipukizi Bora wa Kike na Kiume, Mwanamichezo wa Ngazi ya Shule, Mwanahabari Bora wa Michezo, Mwanamichezo Nguli, Klabu Bora ya Kike na Kiume pamoja na Timu Bora ya Taifa.

“Kamati ya maandalizi imejiandaa kikamilifu kuhakikisha shughuli hii inafanyika kwa mafanikio makubwa katika kuwapongeza na kuwasherehekea wanamichezo waliofanya vizuri kitaifa na kimataifa,” amesema Msitha.

Related Articles

Back to top button