Simba yajilaumu, yajipongeza baada ya sare

DAR ES SALAAM: BAADA ya Simba kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga katika dabi ya Kariakoo, Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, amesema matokeo hayo yana pande mbili; kujilaumu kwa kukosa ushindi na kujipongeza kwa maendeleo ya timu.
Akizungumza baada ya mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Jenerali Isamuhyo jana, Ahmed amesema Simba walikuwa na nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi lakini walishindwa kuitumia ipasavyo.
“Kwetu sisi matokeo yana pande mbili. Kwanza tunajilaumu kwa kushindwa kupata ushindi kwa sababu tayari ushindi ulikuwa mikononi mwetu, lakini tumeshindwa kuuchukua,” amesema.
Ameongeza kuwa pamoja na matokeo hayo, bado kuna sababu ya kujivunia kutokana na kiwango kilichooneshwa na timu hiyo, akieleza kuwa ni tofauti na mechi zilizopita dhidi ya wapinzani wao wa jadi.
“Upande wa pili ni kujipongeza kwa maendeleo ya timu. Tumewahi kupoteza mechi nyingi za dabi ya Kariakoo lakini hatukuwahi kuwa na kiwango kama hiki. Katika mechi sita tulizocheza na mtani, hii ni moja ya mechi ambazo tumetawala mpira licha ya kucheza na mpinzani ambaye ametufunga mara nyingi,” amesema.
Ahmed Ally alibainisha kuwa kufunga mabao mawili dhidi ya Yanga ni ishara ya mabadiliko chanya, akisema kwa muda mrefu walikuwa wakipata ugumu wa kuifumania nyavu timu hiyo.
“Kwa upande wa matokeo ni jambo linalohuzunisha, lakini kwa maendeleo ya timu ni jambo la faraja. Tumepata mabao mawili dhidi ya mpinzani wetu, jambo ambalo kwa muda mrefu lilikuwa changamoto kwetu, hivyo kuna maendeleo makubwa,” amesema.




