CAF na UEFA zasaini makubaliano kuendeleza soka Afrika na Ulaya

VANCOUVER:SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeingia makubaliano ya kihistoria na Union of European Football Associations (UEFA) yenye lengo la kuimarisha ushirikiano, kukuza vipaji na kuendeleza mchezo wa soka katika mabara ya Afrika na Ulaya.

Makubaliano hayo (MoU) yalisainiwa jijini Vancouver, Canada, yakiongozwa na Rais wa CAF, Patrice Motsepe, pamoja na Rais wa UEFA, Aleksander Čeferin.
Akizungumza baada ya utiaji saini huo, Motsepe amesema hatua hiyo ni muhimu katika safari ya kuifanya soka ya Afrika kuwa miongoni mwa bora duniani, akisisitiza kuwa ushirikiano huo utaongeza fursa kwa vijana, wanawake, makocha na waamuzi.
Kwa upande wake, Čeferin alieleza kuwa makubaliano hayo yatafungua milango ya maendeleo ya soka kwa jinsia zote, huku yakilenga pia ustawi wa afya na jamii kupitia mchezo huo.
Makubaliano hayo yatadumu hadi Juni 30, 2031, yakigusa maeneo kadhaa muhimu ikiwemo: Maendeleo ya soka la vijana na wanawake, Programu za kukuza soka na ushirikiano wa muda mrefu, Mafunzo ya makocha na waamuzi, kubadilishana utaalamu na uzoefu wa kiutendaji.
Hatua hiyo inaashiria dhamira ya pamoja ya CAF na UEFA kutumia soka kama chombo cha kuleta umoja, fursa na maendeleo ya kijamii kwa mamilioni ya watu duniani.




