Maema: Uvumilivu na nidhamu vimetupa ushindi

ZANZIBAR: KIUNGO mshambuliaji wa Simba Neo Maema ameweka wazi sababu za ushindi wa mabao 3-0 walioupata dhidi ya Mlandege FC katika mchezo wa nusu fainali michuano ya Muungano, akisema mchezo huo ulikuwa mgumu hasa dakika za mwanzo lakini uvumilivu na nidhamu viliwabeba.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Maema amesema Mlandege waliingia na mpango maalum wa mchezo uliowafanya Simba kushindwa kupata nafasi rahisi kipindi cha kwanza.
“Ilitugharimu sana hasa dakika 20 za mwanzo. Walikuwa na mpangilio wa kujilinda sana, walirudi nyuma wakiwa wachezaji sita, hivyo ilikuwa vigumu kuvunja safu yao ya ulinzi. Tulihitaji kuwa wavumilivu na kubadilisha namna ya kushambulia,” amesema Maema.
Ameongeza kuwa sare ya 0-0 kipindi cha kwanza ilihitaji moyo wa kupambana zaidi kuliko kipaji pekee, akisisitiza kuwa walijua Mlandege wangechoka kadri mchezo unavyoendelea.
“Tulijua tukivumilia na kuendelea kuwachosha, nafasi zitatokea. Ni suala la nidhamu na kupambana zaidi, si kipaji tu,” ameongeza.
Akizungumzia mabao na ushindi huo, Maema amesema walitekeleza kwa usahihi maelekezo ya benchi la ufundi na walifurahia jinsi timu ilivyobadilika kipindi cha pili.
Kuhusu bao alilofunga, kiungo huyo amesema amefurahia kufunga bao hilo akisisitiza kuwa ni sehemu ya majukumu yake kusaidia safu ya ushambuliaji ya Simba.
“Ni kitu ninachofanya mazoezini kila siku, kusaidia washambuliaji na kuisaidia timu kufunga. Nimefurahi kufunga bao zuri,” amesema.
Simba itakutana na Yanga katika mchezo wa fainali Jumatano.




