Mbio za Absa Dar City kumahisha mshikamano na afya njema

DAR ES SALAAM: The Runners Club kwa kushirikiana na benki ya Absa imezindua rasmi mbio za Absa Dar City Marathon 2026 zinazotarajiwa kufanyika Mei 17, 2026 Dar es Salaam.
Hilo ni toleo la sita la mbio hizo, zikitarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki 5,000 kutoka ndani na nje ya nchi, huku zikilenga kuhamasisha mazoezi, mshikamano wa kijamii na afya.
Akizuzungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Makamu wa Rais wa The Runners Club, Godphrey Mindu alisema mashindano ya mwaka huu yatahusisha mbio za kilomita 21, kilomita 10 na kilomita 5.
“Mbio hizo zitafanyika katikati ya jiji la Dar es Salaam, zikitoa fursa kwa washiriki kupita katika vivutio mbalimbali vya kihistoria na kisasa ikiwemo Mnara wa Saa, Askari Monument, Dar es Salaam International Conference Centre (JNICC), Tanzanite Bridge, Coco Beach na Selander Bridge,”alisema.
Alisema lengo kuu la mbio hizo linaendana na dira ya klabu ya kuhamasisha afya kupitia mazoezi ya kukimbia, pamoja na kupunguza magonjwa yasiyoambukiza (NCDs).
Aidha alisema mbio hizo zitaiunga mkono Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa kuchangia vifaa tiba na kemikali.
“Usajili wa kushiriki mbio hizo umefunguliwa rasmi kupitia majukwaa mbalimbali pamoja na mtandao. Washiriki wa ngazi zote, kuanzia wanariadha wa kitaalamu hadi wale wa kawaida, wanahimizwa kujisajili mapema na kushiriki,”aliongeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa benki ya Absa, Aaron Luhanga, alisema mbio hizo si mashindano pekee bali ni jukwaa la kuhamasisha afya bora, umoja na maendeleo ya jamii.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam, Felix Donald, alisema mbio hizo ni muhimu katika kugundua na kukuza vipaji vya wanariadha pamoja na kuhamasisha nidhamu na afya bora.




