Serikali yapiga hesabu za Olimpiki 2028
SERIKALI imelitaka Baraza la michezo la Taifa Tanzania (BMT) kuhakikisha vyama vya michezo vinaleta mipango yao kwa ajili ya kujiandaa na Olimpiki ijayo itakayofanyika mwaka 2028 nchini Marekani.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo,Dkt Sulemani Serera ameyasema hayo katika hafla ya kuaga na kukabidhi bendera timu ya Tanzania itakayoshiriki michezo ya Olimpiki itakayoanza Julai 26 hadi Agosti 11 mwaka huu Paris nchini Ufaransa.
Amesema lengo ni kuandaa timu na kupata idadi kubwa ya wachezaji ambao wanakidhi viwango vya kwenda kushiriki michuano hiyo mwaka 2028 kwa ajili ya kuipeperusha vyema bendera ya Taifa kupitia michezo.
“Mwaka huu tunawakilishwa na wachezaji saba, lengo letu ni kuona mwaka 2028 tunapeleka idadi kubwa ya wachezaji na Serikali itaendelea kushirikiana na Mashirikisho ya Michezo ili kufikia malengo yetu,” amesema Serera.
Pia akaongeza kusema wanahitaji kuweka wachezaji katika mazingira mazuri licha ya changamoto zilizopo ambazo amesema serikali itajitahidi kuzitatua.
Kwa upande wake Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Gulam Abdulla, amesema kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo lazima mchezaji afikie viwango vinavyohitajika na Olimpiki.
“Hatupeleki mchezaji ambaye hajakidhi vigezo vya kushiriki Olimpik. Hawa wote wanaokwenda ni wale ambao wamekidhi vigezo,” amesema Gulam.
Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi amesema maandalizi ya safari hiyo yamekamilika ikiwa pamoja na kupata viza na tiketi kwa ajili ya kusafiria.
Katibu huyo amesema timu hiyo itaondoka kwa makundi ambapo kundi la kwanza litaondoka Julai 22 na kundi la pili Julai 23 huku kundi la mwisho litaondoka Julai 27.